SYRIA

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lapanga kupitisha vikwazo dhidi ya rais wa Syria Bashar Al Assad

Wajumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kupigia kura azimio la kumwekea vikwazo rais wa Syria Bashar Al Assad.

Matangazo ya kibiashara

Azimio hilo linatarajiwa kupigiwa kura Jumatano hii, lakini tayari Urusi imesema kuwa itatumia kura yake ya veto kuzuia kupitishwa kwa azimio lolote dhidi ya rais Assad.

Aidha, baraza hilo linatarajiwa kujadili hatima ya waangalizi wa kijeshi nchini Syria ambao wanamaliza muda wao siku ya Ijumaa.

Licha ya mpatanishi wa kimataifa koffi Annan kuwa katika ziara ya siku mbili nchini Urusi kujaribu kuishawishi nchi hiyo kubadilisha msimamo wake kuhusu machafuko ya Syria, Moscow imeendelea kushikilia msimamo wake kuwa suluhu la Syria liwachiwe raia wa taifa hilo.

Mashambulizi yameendelea kusikika katika Mji Mkuu wa Syria, Damascus kwa siku ya pili mfululizo huku serikali ikiingia kwenye lawama ya kutumia silaha zenye kemikali katika kutekeleza mauaji ya kinyama.

Tuhuma hizi zimetolewa na Balozi wa zamani wa Syria nchini Iraq Nawaf Fares ambaye ameasi serikali na kusema anafahamu kile ambacho kinafanywa na serikali kwenye matumizi ya silaha zenye kemikali.

Machafuko nchini Syria yanaendelea kwa miezi kumi na sita sasa na kusababisha maelfu ya watu kupoteza maisha yao nchini humo.