MISRI-SINAI

Wanajeshi zaidi wa Misri waongezwa kwenye eneo lenye machafuko la Sinai kuimarisha usalama

Wanajeshi wakiwa kwenye hospitali ya mji wa  al-Arish amabko majeruhi wamekuwa wakipelekwa, ulinzi umeimarishwa kwenye eneo hilo na mpakani mwa Sinai
Wanajeshi wakiwa kwenye hospitali ya mji wa al-Arish amabko majeruhi wamekuwa wakipelekwa, ulinzi umeimarishwa kwenye eneo hilo na mpakani mwa Sinai REUTERS/Stringer

Jeshi la Misri limeendelea kutuma vikosi zaidi katika eneo la Kaskazini mwa Sinai ili kuimarisha ulinzi ikiwa ni hatua ya kukabiliana na mashambulizi kama yale ambayo yalisababisha vifo vya askari kumi na sita. 

Matangazo ya kibiashara

Mamia ya wanajeshi pamoja na zana mbalimbali zikiwemo silaha nzito na vifaru vikiwa vimefika eneo la Al Arish ambapo duru za kijeshi zimesema wanapambana na vitendo vya kigaidi kwenye mipaka yake.

Ulinzi huu unaimarishwa wakati ambapo kumekuwa na tetesi ya makundi ya kiislam kujiandaa kutekeleza mashambulizi zaidi ya kujitoa mhanga na kushambulia maeneo ya ukaguzi wa magari kwenye mipaka.

Kuongezwa kwa vikosi hivyo kwenye eneo la Sinai kumeendelea kuongeza hofu ya kiusalama kwenye eneo hilo ambapo wananchi wameanza kuishi kwa wasiwasi kutokana na kuendelea kuongezeka kwa mashambulizi ya kushtukiza.

Hapo jana kumeripotiwa kutokea makabiliano kati ya wanajeshi na watu wasiofahamika kwenye mji wa Sinai ambapo polisi walifanikiwa kuzima jaribio la watu hao ambao hata hivyo hawakuweza kubainika.

Juma hili rais Mohamed Morsi alitangaza kuongezwa kwa wanajeshi kwenye eno hilo na kuahidi Serikali yake kukabiliana na kikundi ama makundi yoyote ya watu ambao wanatumia mwanya wa amani ambayo imeanza kupatikana nchini humo kuvuruga usalama.

Juma hili pia alitangaza kumfukuza kazi aliyekuwa mkuu wa usalama wa taifa na kumteua mkuu mpya na kumuagiza waziri wa ulinzi Field Marshal Hussein Tantawi kuhakikisha usalama narejea kwenye eneo la Sinai.