PAKISTAN-MAREKANI

Maandamano makubwa kufanyika katika nchi za Kiislam baada ya Sarat Ijumaa kupinga filamu inayodhalilisha Uislam

Waandamanaji nchini Pakistan wakieleka kwenye Ubalozi wa Marekani kupinga filamu inayodhalilisha Uislam
Waandamanaji nchini Pakistan wakieleka kwenye Ubalozi wa Marekani kupinga filamu inayodhalilisha Uislam REUTERS/Faisal Mahmood (

Maandamano makubwa yameandaliwa katika nchi za Kiislam Duniani baada ya kufanyika sarat Ijumaa kuendelea kupinga filamu inayomdhalilisha Kiongozi wa Dini hiyo Mtume Muhammad SAW iliyotengenezwa nchini Marekani.

Matangazo ya kibiashara

Vikosi vya usalama katika nchi hizo wamejipanga vilivyo katika kuhakikisha wanakabiliana na maandamano hayo ambayo tangu kuanza kwake yamekuwa yakiishai kwa kushambulia Balozi za Marekani na kuchoma bendera za nchi hiyo.

Serikali ya Pakistan imetangaza leo kuwa siku ya mapumziko kutoa nafasi kwa wananchi kushiriki kwenye maandamano hayo ambayo yanafanyika katika siku iliyopewa jina la “Siku ya Upendo Kwa Mtume Muhammad”.

Washington imekilipa kituo cha Televisheni cha Pakistan kuonesha tangazo la rais Barack Obama ambalo linamuonesha akilaani filamu hiyo inayodhalilisha Uislam na Kiongozi wao Duniani.

Maandamano nchini Pakistan yalianza tangu jana ambapo wananchi wenye hasira walijitokeza mitaani kuonesha hasira zao dhidi ya filamu hiyo iliyosababisha kuuawa kwa Balozi wa Marekani nchini Libya Christopher Stephens.

Serikali ya Pakistan imewataka wananchi kufanya maandamano yao kwa amani kitu ambacho kitafikisha ujumbe duniani kote ya kwamba hawaridhishwi na kile ambacho kimefanywa na Marekani kupitia filamu hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan Hina Rabbani Khar amesema ni siku maalum ambayo inastahili kutumiwa vizuri kabisa na wananchi wote wa Pakistan katika kuonesha wanapinda udhalilishaji dhidi ya Uislam.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton amesisitiza serikali yake haiungi mkono filamu hiyo ambayo inadhalilisha Uislam na watahakikisha hatua zinachukuliwa kwa waliotengeneza.