MAREKANI-IRAN

Rais wa Iran, Ahmadinejad ayashutumu mataifa ya magharibi kuhusu vitisho kuivamia kijeshi nchi yake

Rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad akuhutubia mkutano wa Umoja wa Mataifa siku ya Jumatano
Rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad akuhutubia mkutano wa Umoja wa Mataifa siku ya Jumatano UN Photo/Jennifer S Altman

Rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad ameendelea kuyashutumu mataifa ya magharibi kwa kuendelea kuitishia nchi yake kuivamia kijeshi iwapo itaendelea na mpango wake wa kurutubisha Nyuklia.

Matangazo ya kibiashara

Rais, Ahmadinejad amesema hayo wakati akihutubia mkutano wa mwaka wa Umoja wa Mataifa kwenye hotuba ambayo hata hivyo ilisusiwa na nchi za Marekani na Israel ambazo zimekuwa mkosoaji mkubwa wa sera ya Iran kuhusu Nyuklia.

Kiongozi huyo bila kung'ata maneno amezinyooshea vidole nchi za Marekani na Israel kwa kuendelea kuwa sehemu ya migogoro kwenye mataifa ya mashariki ya kati, na kusisitiza kuwa kamwe nchi yake hatishiki na vitisho vyao.

Rais, Mahmoud Ahmadinejad ametumia mwanya wa hotuba yake kukashifu mpango wa mataifa ya magharibi kuhusu nchi yake, ikiwa ni hotuba yake ya mwisho kwenye Baraza hilo kabla ya kumaliza muhula wake wa urais hapo mwakani.

Ameitaja nchi ya Israel kama nchi yenye msimamo mkali kijeshi kwa kupenda vita zaidi kuliko kutumia diplomasia kumaliza mzozo huku akidiriki kuitaka nchi hiyo kuivamia kijeshi nchi yake.

Siku ya Jumanne rais wa Marekani Barack Obama alitumia hotuba yake kukashifu mpango wa Iran huku akiitaka nchi hiyo kutekeleza maazimio ya Umoja wa Mataifa kuhusu kuisitisha kurutubisha Nyuklia na kamwe hatoiacha nchi hiyo kutengeneza silaha za maangamizi.

Nchi ya Iran inakabiliwa na shinikizo kubwa toka mataifa ya magharibi na Umoja wa Mataifa ambazo zimetangaza vikwazo dhidi ya nchi hiyo kufuatia kuendelea kukataa vinu vyake kukaguliwa na waangalizi wa Umoja wa Mataifa.