AFGHANISTAN-MAREKANI

Wanajeshi 2,000 wa Marekani wameuliwa nchini Afghanistan tangu 2001

Idadi ya wanajeshi wa Marekani waliouawa nchini Afghanistan wakilinda amani na kupambana na kundi la Taliban chini ya majeshi ya kimataifa ya NATO kwa muda wa miaka 11 imefikia 2,000 .

Matangazo ya kibiashara

Idadi hiyo imefikia elfu mbili baada ya kuuliwa kwa mwanajeshi mmoja wa Marekani Mashariki mwa Afghanistan siku ya Jumapili.

Katika hatua nyingine,shambulizi la kujitoa mhanga nchini humo limesababisha mauaji ya watu 14 wakiwemo wanajeshi 3 wa NATO.

Shambulizi hilo lilitokea wakati wakipiga doria katika mji wa Khost siku ya Jumatatu na kusababisha kujeruhiwa kwa watu wengine zaidi ya 30.

Kundi la Taliban limekiri kutekeleza shambulizi hilo na kudai kuuawa kwa wanajeshi 8 na wanajeshi 6 wa Afghanistan.

NATO ina wanajeshi 100,000 wanaopigana na Taliban nchini humo na kulinda amani na wanatarajiwa kuondoka nchini humo kufikia mwaka 2014.

Makabiliano kati ya wanajeshi wa NATO na kundi hilo la Taliban yamesabisha kuuawa kwa watu 347.