Syria

Mabomu ya kujitoa mhanga yasambaratisha maisha ya watu wengi nchini Syria

REUTERS/Murad Sezer

Watu kadhaa wameuawa hii leo nchini Syria baada ya kufanyika mashambulizi mawili ya kujitoa mhanga katika kambi moja ya jeshi la usalama mjini Harasta kaskazini Mashariki mwa mji mkuu wa nchi hiyo Damascus.

Matangazo ya kibiashara

Mkurugenzi wa Shirika la ufuatiliaji wa haki za binadamu, Rami Abdel Rahman amesema kuna idadi kubwa ya watu waliouawa kutokana na mashambulizi hayo.

Hata hivyo hatma ya wafungwa ambao walikuwa wanashikiliwa katika majengo hayo haijulikani mpaka sasa ingawa kuna hofu kuwa huendea wameuawa kutokana na mashambulizi.

Wakati huo huo Vikosi vya Serikali ya Syria vimezidisha mashambulizi zaidi dhidi ya waasi wa jeshi huru la Syria kwenye mji wa Hama ambapo kumeripotiwa vifo vya watu kadhaa.

Wakati mashambulizi hayo yakiendelea kwa mara ya kwanza kiongozi wa baraza la waasi, Abdel Basset Sayda amefanya ziara yake ya kwanza nchini humo kwa kutembelea mji wa Bab al-Hawa ulioko kaskazini mashariki mwa mji wa Idlib kujionea uharibifu uliotokana na machafuko yanayoendelea.

Hofu ya kuzagaa kwa silaha za kemikali nayo imeendelea kutanda huku wachambuzi wa masuala ya siasa wakionya kuhusu mashambulizi ambayo yanaendelea kufanywa na majeshi ya Uturuki ndani ya ardhi ya syria kuwa huenda yakaziingiza nchi hizo kwenye vita.