PAKISTAN

Mtoto aliyeshambuliwa na Taliban Pakistan aendelea kuombewa

©Reuters.

Swala za kumuombea mwanaharakati wa haki za elimu mwenye umri wa miaka 14 Malala Yousafzai zimeendelea nchini Pakistan huku madaktari wakifanikiwa kutoa risasi katika bega lake baada ya kushambuliwa eneo la Mingora kaskazini magharibi mwa Pakistan.

Matangazo ya kibiashara

Malala Yousafzai kwa sasa yupo katika uangalizi maalum huku akipatiwa matibabu na madaktari baada ya kushambuliwa wapiganaji wa kundi la Taliban hiyo jana akiwa katika basi la wanafunzi.

Waziri wa mambo ya ndani wa Pakistan Rehman Malik amesema Malala ataendelea kupatiwa matibabu huko Peshawar mpaka taarifa za madaktari zitakapothibitishwa kama anaweza kupelekwa sehemu nyingine.

Tukio hilo limelaaniwa na wanaharakati wa haki za binadamu na viongozi wengi huku wachambuzi wa siasa za nchi hiyo wakihoji kwa nini serikali imeshindwa kumlinda Malala dhidi ya Taliban.

Malala amekuwa akitetea haki ya elimu kwa mtoto wa kike na amewahi kupata tuzo mbalimbali kutokana na jitihada zake za kuinua elimu na pale alipopinga matakwa ya Taliban katika kuzuia haki ya elimu kwa watoto wa kike.