Syria

Watu 50 wauawa Syria, waasi waendeleza mashambulizi ya kutungua ndege za kijeshi

RFI

Watu zaidi ya 50 wamekufa nchini Syria kufuatia milipuko ya mabomu katika magari huku waasi nao wakiendeleza mashambulizi na kutungua ndege za kijeshi kwa siku mbili mfululizo.

Matangazo ya kibiashara

Waangalizi wa haki za binadamu nchini Syria wameripoti tukio la mashambulizi ya mabomu kwenye eneo la kuhifadhi magari katika mji wa Jamarana wenye idadi kubwa waumini wa dini ya wakristo.

Watu zaidi ya 50 wameuawa huku wengine zaidi ya 120 wakijeruhiwa vibaya katika eneo hilo ambalo limekuwa likilengwa na mashambulizi ya aina hiyo kwa mara nne katika kipindi cha miezi mitatu.

Katika tukio jingine waasi wameshambulia na kutungua ndege ya kivita kaskazini magharibi mwa mpaka wa Syria na Uturuki ikiwa ni siku moja baada ya waasi kutungua helikopta nyingine ya jeshi.

Mashuhuda wa tukio hilo wameeleza kuwa baada ya tukio hilo waasi wa jeshi huru la Syria FSA walimkamata rubani mmoja na kuanza kumshambulia.

Mashambulizi kati ya serikali na wapinzani wa utawala wa Rais Bashar Al Assad yamesababisha vifo vya watu zaidi ya elfu arobaini tangu mwezi machi mwaka jana.