DR-Congo

Waasi wa M23 waendelea kujitoa katika mji wa Goma, Serikali ya Kabila yajipanga kurejesha hali ya utulivu

RFI

Kundi la Waasi la M23 ambalo linashikilia Mji wa Goma kwa karibu juma moja sasa limeendelea kuondoka katika Mji huo kutekeleza amri ambayo imetolewa na Viongozi wa Ukanda wa Maziwa Makuu ICGLR pamoja na Umoja wa Mataifa UN.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hiyo inakuja kipindi hiki ambacho Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC Raymond Tshibanda akiweka bayana anaamini kuna uwezekano wa kumalizwa kwa mgogoro ambao unaendelea katika nchi hiyo.

Waziri Tshibanda amesema licha ya Mji wa Goma kuendelea kuwa katika hali tete lakini wao wanaendelea na mchakato wa kuhakikisha hali ya utulivu inarejea katika nchi hiyo kama ilivyokuwa awali.

Kauli ya Tshibanda inakuja kipindi hiki ambacho Marekani ikilitaka Kundi la Waasi la M23 kuondoka mara moja Goma na kurejea walipokuwepo mwezi Julai mwaka jana kauli iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje Hillary Clinton.

Tayari Kundi la Waasi la M23 limesema litatangaza safu ya viongozi wake akiwemo Gavana atakayebaki katika Mji wa Goma huku Gavana wa Serikali ya Kinshasa Julian Paluku akisema atarejea eneo hilo pale Jeshi la FARDC litakapofika.