AFGHANISTAN

Wapiganaji wa Taliban washambulia uwanja wa ndege ambao ni msingi wa vikosi vya NATO

Reuters

Kundi la wapiganaji wa Taliban limevamia na kushambulia uwanja wa ndege wa Afghanistan ambao ni msingi mkubwa wa vikosi vya umoja wa kujihami wa nchi za magharibi NATO.

Matangazo ya kibiashara

Tayari kundi hilo limekiri kuhusika na mashambulizi yaliyojiri leo jumapili asubuhi tukio ambalo pia limethibitishwa na serikali ya Afghanistan.

Tukio la kushambuliwa kwa uwanja wa ndege ni la pili kutekelezwa na Taliban kwa mwaka huu likifuatia shambulizi la kwanza la mwezi April.

Ripoti za awali zimebaini kuwa Maafisa Usalama watatu wa serikali ya Afghanistan wameuawa na wengine kujeruhiwa katika vikosi vyao.

Kundi la kiislamu la Taliban limekuwa likipingana na serikali kwa takribani miaka 11 wakati serikali ikipata msaada wa vikosi vya kujihami vya nchi za magharibi NATO katika kukabiliana na wapiganaji hao.