Syria-Uturuki

Uturuki yaonywa juu ya mpango wa kupeleka makombora na wanajeshi katika mpaka wake na Syria

Mkuu wa vikosi vya majeshi nchini Iran Generali Hassan Firouzabadi ameionya Uturuki dhidi ya mpango wa kupeleka makombora na wanajeshi katika mpaka wake na Syria, suala ambalo amesema ni mpango wa nchi za magharibi katika kutaka kuleta vita ya dunia.

Matangazo ya kibiashara

Mkuu huyo amesema kuwa hatua hiyo ni hatari kwa usalama wa kila mmoja suala ambalo pia linaungwa mkono na washirika wa karibu wa utawala wa Rais wa Syria Bashar Al Assad.

Vikosi vya kujihami vya nchi za magharibi NATO vilikubali kupeleka makombora katika mpaka wa Uturuki na Syria ili kuimarisha ulinzi na kuzuia mapigano hayo yasiathiri eneo la Uturuki.

Mapigano kati ya wapinzani na majeshi ya serikali ya Syria yameingia katika mwaka wake wa pili hivi sasa na kusababisha zaidi ya vifo vya watu elfu 40.