JAMHURI YA AFRIKA YA KATI

Waasi wa Seleka wakubali kufanya mazungumzo na Serikali ya Bangui na kusitisha kuteka Miji zaidi

Wanajeshi wa Jeshi la Serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati FACA wakifanya doria kwenye Jiji la Bangui
Wanajeshi wa Jeshi la Serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati FACA wakifanya doria kwenye Jiji la Bangui REUTERS/Luc Gnago

Waasi wa Seleka ambao wanapambana na Serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati wametangaza kusitisha mpango wao wa kuendelea kusonga mbele na kuteka Miji zaidi na badala yake wapo tayari kwa mazungumzo na serikali ya Rais Francois Bozize.

Matangazo ya kibiashara

Uamuzi wa Waasi wa Seleka unakuja baada ya Kikosi cha Kulinda Amani cha Afrika ya Kati FOMAC kuingia Bangui kwa lengo la kulinda maeneo ambayo bado yapo chini ya serikali kudhibiti yasiangukie kwenye mikono ya Waasi.

Msemaji wa Waasi wa Seleka Eric Massi ndiye ametangaza utayari wa Kundi lao kurejea kwenye meza ya mazungumzo na Serikali ya Bangui ambayo sasa yamepangwa kufanyika nchini Gabon katika Mji Mkuu wake Libreville.

Massi ametangaza hatua yao ya kusitisha harakati zao zote za kusonga mbele na badala yake wanajiandaa kwa mazungumzo hayo na sasa wanaajipanga kupeleka Ujumbe wao huko gabon kwa mazungumzo.

Mazungumzo hayo yanatarajiwa kuanza tarehe nane ya mwezi huu januari ambapo Msuluhishi kwenye mchakato huo anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Congo Denis Sassou Nguesso.

Msemaji huo wa Waasi wa Seleka amesema wao mara zote wamekuwa mstari wa mbele kuhitaji amani na ndiyo maana walishaweka bayana msimamo wao hawatofika Bangui licha ya kuishikilia Miji mingine kadhaa.

Uamuzi wa Waasi wa Seleka unakuja baada ya Kikosi cha FOMAC kutoa onyo kali kwa Waasi wa Seleka wenye mpango wa kuuteka Mji wa Bangui kutothubutu kufanya hivyo kwani watasambaratishwa vilivyo na Kikosi hicho imara.

Kamanda wa Kikosi cha FOMAC Jenerali Jean-Felix Akaga ndiye ametoa onyo hilo kwa Waasi wa Seleka na kuwataka kutokuwa na mawazo ya kuuchukua Mji wa Damara ambao unashikiliwa na Majeshi hayo wakisaidia Jeshi la serikali.

Katika hatua nyingine Rais Bozize amemfuta kazi mwanaye Jean-Francis Bozize ambaye alikuwa anahudumu kwenye nafasi ya Waziri wa Ulinzi na ameamua kuchukua nafasi hiyo mwenyewe huku pia akimtimua Mkuu wa Majeshi Guillaume Lapo.