VENEZUELA-CUBA

Rais Chavez anakabiliwa na maradhi ya mapafu akiendelea kupata tiba ya saratani nchini Cuba

Rais wa Venezuela Hugo Chavez ameanza kusumbuliwa na maradhi ya mapafu baada ya upasuaji wa saratani
Rais wa Venezuela Hugo Chavez ameanza kusumbuliwa na maradhi ya mapafu baada ya upasuaji wa saratani

Serikali ya Venezuela imewatuhumu wapinzani na vyombo vya habari nchini humo kutumia hali ya afya ya Rais Hugo Chavez kutaka kuzorotesha hali ya utulivu katika nchi hiyo kipindi hiki ambacho Kiongozi huyo akiendelea kupata matibabu ya saratani huko Cuba.

Matangazo ya kibiashara

Makamu wa Rais wa Venezuela na mndani wa Rais Chavez, Nicolas Maduro ndiye ambaye ametoa agizo la kutolewa onyo kwali kwa wapinzani na vyombo vya habari kuachana kabisa na kutumia ugonjwa wa kiongozi wao kama mtaji wa kutaka kuleta machafuko.

Maduro baada ya kurejea amewaambia wananchi wa Venezuela wale ambao wanataka kuzorotesha usalama wa nchi hiyo hawatoweza sababu mara zote wamekuwa pamoja na raia na sasa umoja umezidi.

Makamu wa Rais amesisitiza wale ambao wanataka kutumia maradhi ya Rais Chavez kama mtaji wao kisiasa na kuleta machafuko hawatoachwa na badala yake watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi hiyo.

Waziri wa Habari Ernesto Villegas amejitokeza kwenye Televisheni ya Taifa kuwatoa hofu wananchi wa Taifa hilo na kuwaeleza kwa sasa Rais Chavez anakabiliwa na tatizo la mapafu linalochangia apumue kwa shida.

Waziri Villegas hakuishia kutoa taarifa tu bali akatoa onyo kali kwa vyombo vya habari kutoshiriki kwa namna yoyote kwenye vita ya kisaikolojia ambayo imeanzishwa kipindi hiki ambacho Rais Chavez anatibiwa huko Cuba.

Naye Spika wa Bunge Diosdado Cabello aliyekuwa nchini Cuba kumjulia hali Rais Chavez amesema wapinzani wasiwe na matumaini ya kwamba kutakuwa na mabadiliko ya utawala kwani kiongozi wao atarejea ofisini punde tu.

Rais Chavez yupo nchini Cuba kwa majuma zaidi ya matatu sasa tangu afanyie upasuaji wa saratani ambayo imekuwa inamsumbua lakini wakati akiendelea na matibabu kumekuwa na maradhi mengine nyemelezi yakimkumba.