MALI-UFARANSA-ETHIOPIA

Majeshi ya Ufaransa na Mali yaendelea na doria katika Mji wa Timbuktu huku Mkutano wa kuchagia fedha kusaidia mapigano ukifanyika Ethiopia

Msikiti uliopo katika Mji wa Timbuktu, Mali eneo ambalo limechukuliwa na Majeshi ya Ufaransa na Mali
Msikiti uliopo katika Mji wa Timbuktu, Mali eneo ambalo limechukuliwa na Majeshi ya Ufaransa na Mali Wikimedia Commons

Majeshi ya Ufaransa na Mali yanaendelea kufanya doria katika Mji uliojaaliwa misitu mingi wa Timbuktu baada ya kupata mapokezi ya kishujaa kutoka kwa wakazi wake baada ya Makundi ya Kiislam ambayo yalikuwa yameweka makazi yao kwa kipindi cha miezi tisa kuondoka. Doria hii ni harakati za kufanya uchunguzi kama Wapiganaji wa Makundi ya Kiislam wameendelea kujihifadhi katika maeneo mbalimbali kwenye Mji wa Timbuktu baada ya kuingia kwenye eneo hilo bila ya kukabiliwa na upinzani wa aina yoyote.

Matangazo ya kibiashara

Wananchi wa Mji wa Timbuktu wameonesha furaha yao pindi tu majeshi ya Ufaransa na yale ya Mali yalipofanikiwa kuingia katika Mji huo ikiwa ni ishara ya kuurejesha tena kwenye mikono ya serikali baada ya kuanguka kwa wapiganaji hao.

Wakazi wa timbuktu wamewapokea wanajeshi wa Ufaransa na Mali kama mashujaa huku wakiimba “Mali, Mali, Mali” na kupeperusha bendera za mataifa hayo mawili ambayo yamekuwa mstari wa mbele kuyatokomeza makundi hayo ya Kiislam.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande amekiri hatua ya kuuchukua Mji wa Timbuktu ni hatua kubwa katika mapambano yao ya kigaidi ambayo wameyaanzisha katika eneo la Kaskazini mwa Bara la Afrika.

Hollande amesisitiza wana wakati mgumu katika mapambano hayo dhidi ya ugaidi kutokana na vitendo hivyo kukita mizizi katika eneo la Kaskazini mwa Bara la Afrika lakini wamekuwa na mwanzo mzuri.

Katika kufanikisha harakati za kumaliza makundi ya kigaidi Kaskazini mwa Mali tayari Japan imetangaza kutoa msaada wa dola milioni 120 ikiwa ni sehemu ya kusaidia kuimarisha hali ya usalama katika eneo la Sahel.

Msaada huo unakuja ikiwa ni siku kumi baada ya raia wa Japan kupoteza maisha kwenye shambulizi la utekeaji nyara lililotekelezwa nchini Algeria kwenye kiwanda kimoja cha kuzalisha gesi.

Umoja wa Afrika AU nao umeandaa mkutano maalum ukishirikisha mataifa ya Magharibi kuchangia pesa kwa ajili ya kusaidia vita vinavyoendelea Kaskazini mwa Mali lengo likiwa ni kumaliza Makundi ya Kiislam ambayo wamekuwa wakiyaita ya kigaidi.