Tunisia-Maandamano

Upinzani nchini Tunisia waitisha maandamano baada ya kifo cha kiongozi mkuu wa upinzani

Maandamano nchini Tunisia kupinga mauaji ya kiongozi wa upinzani
Maandamano nchini Tunisia kupinga mauaji ya kiongozi wa upinzani

Vyama vinne vya upinzani nchini Tunisia vimewatolea wito wananchi wa Taifa hilo kufanya mgomo wa jumla baada ya kutokea mauaji ya kiongozi mkuu wa upinzani Chokri Belaid. Mauaji hayo ya kwanza kutokea tangu kufanyika  mapinduzi yaliomuondowa madarakani rais Ben Ali na kuzua ghasia za maandamano hadi kushambulia majengo ya chama madarakani cha Ennahda.

Matangazo ya kibiashara

Hayo yanajiri wakati mataifa kadhaa ulimwenguni yamelaani vikali mauaji hayo ya kiongozi wa upinzani. Nchini Canada, mamia ya watu walikusanyika jana mjini Montreal wakionesha kughadhabishwa na kitendo cha kushambuliwa kwa risasi na kuuawa kwa Kiongozi wa upinzani nchini humo, Chokri Belaid.

Muungano wa Raia wa Tunisia waishio nchini Canada waliounga mkono Harakati za kuuangusha utawala wa aliyekuwa Kiongozi wa Tunisia Zine Al Abidin Ben Ali, wameshutumu Serikali ya sasa kushindwa kupambana na vitendo vya Rushwa na uhalifu.

Jijini Tunis jana baada ya kutokea mauaji ya kiongozi huyo wafuasi wa chama chake walivamia majengo ya chama madarakani katika maeneo mbalimbali na kuyateketeza kwa moto, huku wakikituhumu chama hicho kwamba ndicho kilichohusika na kifo cha kiongozi huyo.

Rais wa Tunisia Moncef Marzouk alilazimika kufupisha safari yake nchini Ufaransa na Misri ambako alitakiwa kushiriki katika mkutano wa jumuiya ya nchi za kiarabu, na kurejea nchini. Rais Moncef alionyesha maskitiko yake kutokana na kifo cha kiongozi huyo wa upinzani ambae alimuita kuwa rafiki yake wa muda mrefu.

Akizungumza na vyombo vya habari rais Moncef Marzouk amesema kwamba mauaji hayo ni ujumbe kwa serikali, ujumbe ambao hautopokelewa, na kwamba wataendelea kufichua uhalifu na kuendeleza sera ya uongozi wake hadi kufikia kwenye mafaanikio.

Kiongozi wa Upinzani, Belaid anatarajiwa kuzikwa siku ya ijumaa baada ya swala ya ijumaa, ambapo kifo chake kimesababisha maandamano huku waandamanaji wakishambulia majengo ya Serikali ya chama cha Enhada.