Wanajeshi wa Mali wanawasaka waasi wa MUJAO nyumba hadi nyumba
Wanajeshi wa Mali wanafanya msako wa nyumba hadi nyumba kuwasaka waasi wa Kiislamu wa kundi la MUJAO baada ya kuzuka kwa mashambulizi ya kustukiza katika mji wa Gao mwishoni mwa Juma lililopita.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Shambulizi la bomu pia limetikisa mji huo siku ya Jumatatu saa chache baada ya kundi la kiislamu kukabiliana na wanajeshi wa Ufaransa na Mali katika mji huo.
Makabiliano kati ya wanajeshi wa Ufaransa na waasi hao yalizuka siku ya Jumapili huku wanajeshi wa Ufaransa wakisema wamefanikiwa kuwaua baadhi ya waasi hao katika makabiliano hayo.
Kundi la waasi la MUJAO limekiri kuhusika na shambuzli hilo na kusema litaendelea na mashambulizi zaidi dhidi ya wanajeshi hao wa Ufaransa kwa kutumia bomu za ardhini.
Inaelezwa kuwa waasi hao walivuka mto Niger na kufaulu kuingia mjini Gao na kuanza mashambulizi hayo dhidi ya vikosi vya kijeshi kutoka Ufaransa na Mali bila kutarajiwa.
Tangu kuanza kwa oparesheni ya kijeshi dhidi ya waasi hao ikiongozwa na majeshi ya Ufaransa na Mali, kumekuwa na makabiliano kati ya waasi na wanajeshi hao lakini hii ndio mara ya kwanza kumetokea na mashambulizi haya ya kushtukiza.
Ufaransa wiki iliyopita ilitangaza kuwa ilikuwa inawasaka waasi hao katika Milima ya Kaskazini mwa nchini hiyo baada ya kufaulu kuwaondoa katika miji waliyokuwa wanathibti kama Kidal na Timbukutu.
Majeshi ya Umoja wa Afrika yanatarajiwa kuachiwa jukumu hilo la kulinda amani na kupambana na waasi hao wa Kiislamu kuanzia mwezi ujao wa tatu watakapoanza kuondoka Kaskazini mwa nchi hiyo.
Ufaransa pia inataka baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio la kutuma majeshi ya kulinda amani Kaskazini mwa nchi hiyo.