Newyork-Korea Kaskazini

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lalaani Korea Kaskazini kwa jaribio la zana za Nyuklia

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani vikali hatua ya serikali ya Korea Kaskazini kufanya jaribio la tatu la zana zake za Nyuklia.

Matangazo ya kibiashara

Marekani ambayo ni mwanachama wa Baraza hilo inataka serikali ya Pyongyang kuwekewa vikwazo zaidi kutokana na jaribio hilo ambalo wanasema limevunja maazimio la Baraza hilo yanayozuia serikali hiyo kufanya jaribio  lolote.

China ambayo ni mshirika wa karibu wa Korea Kaskazini pia imeungana na mataifa mengine kulaani kitendo hicho na kumhoji Balozi wake mjini Beijing kutoa maelezo ya kina kuhusu uamuazi wa serikali yake kutekeleza jaribio hilo.

Urusi kupitai Balozi wake katika Baraza hilo la Umoja wa Mataifa Sergei Lavrov amesema hatua hiyo ya Pyongyang inaonesha namna gani inavyopuuza maazimio ya baraza hilo .

Mataifa kama Japan, Korea Kusini na China sasa yanahofia usalama wa watu wake kutokana na majaribio ya mara kwa mara ya Korea Kaskazini na wiki iliyopita Korea Kusini ilikuwa imeonesha hofu kuwa Korea Kaskzini ingejaribu zana zake.

Tayari Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ameshtumu hatua hiyo anayosema imevunja azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kufanya jaribio hilo.

Korea Kaskazini awali ilifanya majaribio ya zana zake mwaka 2006, 2009 na mwezi Januari ilitangaza kuwa itafanya majaribio yake wakati wowote licha ya onyo kutoka kwa Umoja wa Mataifa.

Jaribio la Korea Kaskazini limezua hali ya wasiwasi katika mataifa jirani kama Japan na Korea Kusini huku viongozi wanaohusika na usalama wakikutana kujadili tahadhari inayoweza kuchukua.