EU

Mawaziri wa Kilimo wanakutana kujadili uuzwaji wa nyama ya farasi barani Ulaya

Mawaziri wa Kilimo kutoka Mataifa ya Ulaya wanakutana mjini Brussels nchini Ubelgiji kujadili kashfa ya uuzwaji wa nyama ya farasi katika mataifa 16 katika Umoja huo.

Matangazo ya kibiashara

Kamishena anayehusika na maswala ya afya katika Umoja huo Tonio Borg atakuwa anawaongoza Mawaziri hao kutatua tatizo hilo na kujaribu kuwahakikishia wateja wa nyama barani Ulaya kuwa nyama wanayokula ni salama.

Siku ya Jumanne,  polisi walivamia kichinjio kimoja nchini Uingereza kilichokuwa kinashukiwa kuuza nyama ya farasi na kuzua mjadala mkubwa nchini humo.

Kugundulika kwa uuzwaji wa nyama hiyo kumezua hofu kwa wateja wa nyama katika Umoja huo wa Ulaya kuhusu usalama wa nyama wanayonunua katika maduka makubwa katika mataifa hayo 16.

Serikali ya Romania imejitokeza waziwazi na kukanusha taarifa kuwa nyama hiyo ya farasi ilitokea nchini humo na haijakuwa ikibainishwa kutofautisha na nyama nyingine.

Mawaziri kutoka Uingereza, Ufaransa, Ireland, Luxembourg , Poland, Romania na Sweden wanashiriki katika mazungumzo hayo huku ikitarajiwa kikubwa kinachozungumziwa ni namna ya kuweka usalama wa vyakula vya kopo vilivyo na nyama vinavyouzwa barani humo.

Wataalam wa afya wanaonya kuwa kula nyama ya farasi ni hatari kwa afya ya binadamu kutokana na dawa zinazotumiwa kutibu farasi hao ni sumu.