Umoja wa Ulaya wataka nyama kupimwa kabla ya kuuzwa
Umoja wa Ulaya unatoa wito kwa mataifa katika muungano huo kufanya uchunguzi wa kina kuhusu nyama inayouzwa katika mataifa mbalimbali barani humo na kuhakikisha kuwa si nyama ya farasi.
Imechapishwa:
Mawaziri wa Kilimo kutoka Umoja huo wamependekeza kufanyika kwa vipimo vya DNA kwa nyama katika mataifa hayo ili kuhakikisha kuwa nyama inayouzwa ni ya ng'ombe.
Mataifa yaliyoathiriwa zaidi na hali hiyo ni pamoja na Uingereza na Ufaransa miongoni mwa mengine 10 yaliyokuwa yanatuhumiwa kuhusika na biashara hiyo ya uuzwaji wa nyama hiyo na kuitaja kama ya ng'ombe.
Uingereza mojawapo ya nchi ambayo imekuwa ikishuhudia kashfa hiyo, imesema kuwa itamchukulia hatua yeyote atakayepatikana kuuza nyama ya farasi badala ya ng'ombe.
Kashfa hiyo imezua maswali barani Ulaya ikiwa taasisi zinazoshughulikia usalama wa chakula unatekeleza majukumu yake ipasavyo.
Tayari maduka makubwa katika mataifa mbalimbali barani humo ambayo yamekuwa yakiuza bidhaa za nyama wameziondoa kwa hofu ya kuuza nyama ya farasi.
Pia kumependekezwa kuwa nyama inayosafirishwa kutoka taifa moja hadi nyingine barani humo ibainishwe wazi inatoka taifa gani huku Romania ikikanusha vikali kuwa ilikuwa ya kwanza kuuza nyama ya farasi badala ya ng'ombe.
Madaktari wanaonya kuwa ulaji wa nyama ya farasi unaweza kuwa hatari kwa afya ya mlaji kutokana na chanjo inayopewa farasi huyo.