UN-IRAN

Wajumbe wa Umoja wa Mataifa na Iran watofautiana tena kuhusu mradi wa Nyuklia

Kiongozi wa Shirika la Kimataifa Umoja wa Mataifa linaloshughulika na maswala ya Atomic IAEA Herman Nackaerts amesema mazungumzo kati ya shirika hilo na serikali ya Iran yamekosa kufikia muafaka kuhusu uwezekano wa shirika hilo kuchunguza mitambo yake ya Nyuklia.

Matangazo ya kibiashara

Nackaerts amesema walizungumza kwa kirefu na serikali ya Tehran lakini hawakuafikiana kuhusu uwezekano wa kuendelea na mpango wao wa kuchunguza mitambo hiyo huku akiahidi wataendelea kufanya mazungumzo kuona ikiwa mwafaka utafikiwa.

Hata hivyo, mwakilishi wa Iran katika shirika hilo la IAEA Ali Asghar Soltanieh amesema licha ya tofauti kuibuka kati ya wajumbe hao, kwa upande mwingine wameafikiana kukutana tena ili kuendelea na mazungumzo hayo.

Mazungumzo kati ya maafisa wa IAEA na serikali ya Iran kwa kipindi kirefu haijakuwa yakifua dafu huku serikali ya Tehran ikisema kuwa shirika hilo linatekeleza matakwa ya mataifa ya Magharibi.

Mazungumzo haya yanakosa kupata mwafaka huku mkutano kati ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani yakiwemo Marekani, China, Urusi, Uingereza ,Ufaransa na Ujerumani ukipangwa kufanyika  tarehe 26 mwezi huu wa pili nchini Kazakistan kuzungumzia mradi wa Iran kuhusu Nyuklia.

Iran imeendelea kukanusha tuhma za mataifa ya Magharibi kuwa mpango wake wa nuclear ni kutengeza silaha za maangamizi mradi ambao wanasema ni wa amani.

Israel imeendelea kutoa wito kwa Marekani kuongoza katika kuiwekea vikwazo zaidi Iran ili kuikomesha kuendelea na mradi huo wanaosema ni hatari kwa usalama wao.