DRCongo - UN

Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu amani nchini DRCongo kusainiwa kabla ya mwishoni mwa mwezi Februari

Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Augustin Matata Ponya amesema mkataba wa Umoja wa Mataifa utakaosaidia kurejesha hali ya amani na utulivu Mashariki mwa nchi hiyo utasainiwa kabla ya kufikia mwishoni mwa mwezi wa Februari.

Augustin Matata Ponyo
Augustin Matata Ponyo
Matangazo ya kibiashara

Matata Ponyo ameyasema hayo baada ya ziara yake katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kukutana na Katibu Mkuu Ban Ki Moon na viongozi wa serikali ya Marekani kujadili kuhusu amani nchini mwake.

Marekani imekubali kuisaidia DRC na  kuhakikisha usalama na utulivu vinatawala katika eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa madini ambako kumekuwa kukishuhudiwa  mapigano na kuzuka kwa makundi ya uasi.

Ponyo ameongeza kuwa Ban Ki Moon amemhakikishia kuwa hatua kubwa zimepigwa na mkataba huo utasainiwa kabla ya kufikia mwisho wa mwezi huu.

Viongozi wa Umoja wa Afrika walisita kusaini  mkataba huo  wa makubaliano ya amani  wiki kadhaa zilizopita jijini Addis Abeba nchini Ethiopia, kwa kile walichokisema kuwa hawakushauriwa.

Huku mkataba huo ukisubiriwa bado kuna mvutano  huko jijini Kampala Uganda baina ya waasi wa M23 na viongozi wa serikali ya Kinshasa ambao hadi sasa hawajafikia mwafaka kuhusu mazungumzo yao ya amani.