TANZANIA

Padri wa Kanisa Katoliki auawa kwa kupigwa risasi visiwani Zanzibar nchini Tanzania

Jeshi la polisi visiwani Zanzibar nchini Tanzania linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki katika eneo la Mtoni mkoa wa Mjini Magharibi. Padri Mushi alipigwa risasi kichwani jumapili hii wakati alipokuwa akienda kuongoza misa katika kanisa la Betras ambapo alifariki muda mfupi baada ya kufikishwa katika hospitali ya Mnazi mmoja visiwani humo.

© RFI
Matangazo ya kibiashara

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa viongozi wa kanisa hilo na kutoa wito kwa Watanzania hususani waumini wa Kanisa Katoliki kuwa watulivu wakati ikishughulikia tukio hilo kwani hakuna mtu ama kikundi cha watu kinachoruhusiwa kuvuruga amani ya nchi ya Tanzania.

Tarehe 25 mwezi desemba mwaka jana Padri Ambrose Mkenda wa Parokia ya Mtakatifu Michael Mpendaye visiwani humo naye alinusurika kifo baada ya kupigwa risasi na kujeruhiwa vibaya wakati akirejea nyumbani kwake baada ya kutoka kanisani kuhudhuria misa.

Aidha kiongozi mwingine wa dini ya kiislamu ambaye ni Msaidizi wa Mufti wa Zanzibar, Shekh Fadhil Soraga naye alimwagiwa tindikali na watu wasiojulikana mwaka jana na kwenda nchini India kwa matibabu zaidi.

Vitendo vya kushambuliwa kwa viongozi wa dini na uchomaji wa nyumba za ibada vimekuwa vikijitokeza nisiwani Zanzibar na serikali ya Tanzania imekuwa ikimea wahusika ambao wanavuruga amani ya Taifa.

Jeshi la polisi nchini Tanzania limekemea vitendo hivyo na limeahidi kuimarisha usalama katika maeneo mbalimbali wakati uchunguzi wa kina ukiendelea ili kubaini chanzo cha mauaji ya hivi karibuni.