VENEZUELA-CUBA

Kiongozi wa Venezuela Kamanda Chavez arejea nyumbani baada ya kupata matibabu ya saratani nchini Cuba

Kiongozi wa Venezuela Hugo Chavez akiwa na mabinti zake wawili wakati akiwa anapata matibabu nchini Cuba
Kiongozi wa Venezuela Hugo Chavez akiwa na mabinti zake wawili wakati akiwa anapata matibabu nchini Cuba REUTERS/Ministry of Information/Handout

Kiongozi wa Venezuela Kamanda Hugo Chavez amerejea nyumbani mapema jumatatu baada ya kupatiwa matibabu ya saratani yaliyodumu kwa majuma zaidi ya mawili nchini Cuba. Taarifa ya Kamanda Chavez kurejea nchini Venezuela imepatikana kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter ambapo mwenyewe ameandika “Tumerejea kwa mara nyingine katika Taifa letu”. Kurejea nyumbani kwa Kamanda Chavez kumewashtua wengi kutokana na hivi karibuni akionekana kwenye picha zinazomuonesha yeye na mabinti zake akiendelea kupata matibabu huko Cuba.

Matangazo ya kibiashara

Kamanda Chavez kwenye ukurasa wake wa Twitter pia ameandika “Asante Mungu. Asanye watu wangu mnaonipenda. Tunaendelea na matibabu tukiwa hapa” umesomeka ukurasa wa Chavez mapema hii leo.

Punde baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege amepelekwa katika Hospital ya Kijeshi inayotambulika kwa jina la Carlos Avarela ambako ataendelea kupatiwa matibabu zaidi baada ya kutibiwa kwa miezi zaidi ya miwili huko Cuba.

Mkwe wa Kamanda Chavez ambaye pia ni Waziri wa Sayansi na Teknolojia Jorge Arreaza amethibitisha kurejea nyumbani kwa Kiongozi huyo ambaye ataendelea na matibabu yake ya saratani.

Makamu wa Rais Nicolas Maduro amekiri Kamanda Chavez kurejea nyumbani mapema hii leo na ataendelea kutibiwa kwani hali yake imeanza kuimarika tofauti na ilivyokuwa baada ya kufanyika operesheni ya saratani.

Kamanda Chavez mwenye umri wa miaka 58 kwenye ujumbe wake alioutuma kwenye Twitter amewashukuru Viongozi wa Cuba akiwemo Fidel Castro na Rais wa Taifa hilo Raul Castro kwa ushirikiano waliompa.

Kiongozi huyo wa Venezuela amewashukuru madaktari na wauguzi ambao wamekuwa wakimpatia huduma kwa kipindi chote alichokuwa anapatiwa matibabu huko Cuba na amewaomba wananchi kuendelea kushikamana.

Chavez amesema anamtegemea Yesu na ana imani kwa nguvu zake atapona na taifa hilo litashinda majaribu ambayo inalipitia kwa sasa na amekiri anawapenda sana wananchi wa Venezuela.