SYRIA

Lakhdar Brahimi azitaka pande zinazohasimiana nchini Syria kuanzisha mazungumzo kumaliza umwagaji wa damu

Mpatanishi wa Mgogoro wa Syria Lakhdar Brahimi ambaye ametaka pande zinazohasimiana kufanya mazungumzo kusaka suluhu
Mpatanishi wa Mgogoro wa Syria Lakhdar Brahimi ambaye ametaka pande zinazohasimiana kufanya mazungumzo kusaka suluhu REUTERS/Khaled al-Hariri

Mpatanishi wa Mgogoro wa Syria anyaetambulika na Umoja wa Mataifa UN na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Lakhdar Brahimi ametaka mazungumzo yafanyike baina ya Wapinzani na Ujumbe uliokubalika kutoka Damascus ili kupata suluhu ya machafuko ya miezi ishirini na tatu.

Matangazo ya kibiashara

Brahimi ametaka mazungumzo hayo yafanyike haraka iwezekanavyo ili kukabiliana na umwagaji wa damu uliokithiri katika nchi ya Syria kutokana na mapigano baina ya wapinzani na wanajeshi watiifu kwa serikali ya Rais Bashar Al Assad.

Mpatanishi wa Mgogoro wa Syria, Brahimi amesema mazungumzo hayo yatasimamiwa na Umoja wa Mataifa UN bila ya kueleza ni wapi hasa yatafanyika lakini amezitaka pande zote kushiriki kwenye mchakato huo wa kumaliza umwagaji wa damu.

Kauli ya Brahimi ameitoa kwenye mkutano wake na waandishi wa habari akiwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Nabil El Araby na kutumia muda wake kuzisihi pande zote kushiriki mazungumzo hayo.

Brahimi bila ya kung'ata maneno akaeleza msimamo wake ni kutaka kuona pande hizo zinaanza mazungumzo hayo ambayo kwa mara ya kwanza yatafanyika katika ofisi ya Umoja wa Mataifa UN.

Mpatanishi huyo amesema kitendo cha Mkuu wa Muungano wa Upinzani wa Syria Mouaz Al Khatib cha kutaka mazungumzo na serikali ya Damascus kina lengo jema kwa nchi hiyo na huenda kikasaidia kumaliza umwagaji wa damu.

Licha ya Brahimi kuendelea kutaka kufanyika kwa mazungumzo baina ya pande hizo mbili lakini ameshindwa kueleza kama uumbe wa serikali ya Damascus umekubali kushiriki au la hadi sasa.

Mapigano yenye lengo la kuing'oa madarakani serikali ya Rais Assad yamesabbaisha zaidi ya watu 60,000 kupoteza maisha katika kipindi cha miezi 23 ya mfarakano huo baina ya serikali na upinzani.