PAKISTAN

Umoja wa Mataifa UN umelaani vikali mauaji ya Washia huko Pakistan na kutaka hatua za haraka kuchukuliwa kudhibiti

Waumini Washia waliouawa nchini Pakistan kwenye mashambulizi ambayo yametekelezwa mwishoni mwa juma
Waumini Washia waliouawa nchini Pakistan kwenye mashambulizi ambayo yametekelezwa mwishoni mwa juma Reuters

Umoja wa Mataifa UN umelaani vikali mauaji yanayoendelea dhidi ya wafuasi wa Kishia ambao waumini 81 wamepoteza maisha kwenye shambulizi lililotekeleza Kusini Magharibi mwa Pakistan na kutaka Mamlaka zichukua hatua za haraka kukabiliana nayo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon amesema kutekelezwa kwa mashambulizi mawili ya kujitoa mhanga yaliyofanyika katika eneo la Quetta yanasikitisha na yanastahili kudhibitiwa.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa Katibu Mkuu Martin Nesirky amesema mashambulizi dhidi ya jamii ndogo ya Washia nchini Pakistan hayakubaliki na lazima juhudi zaidi zifanyike kuwabaini wale ambao wamekuwa wakitekeleza matukio hayo.

Serikali ya Pakistan imetakiwa kuhakikisha inaondoa mgogoro wa kidini ambao unaendelea katika nchi hiyo kwani mauaji hayo yanaweza kuwa chachu ya kuharibika kwa utulivu wa taifa hilo.

Karipio la Umoja wa Mataifa UN limekuja kipindi hiki ambacho waandamanaji wamejitokeza mitaani kupinga mauaji hayo ambayo yameanza kuwagawa wananchi wa Taifa hilo.

Mashambulizi hayo katika eneo la Quetta yamesababisha majeruhi ya watu 178 kitu ambacho kimeongeza uhasama baina ya Washia na Wasunni ambao ndiyo wengi nchini Pakistan.

Wanawake zaidi ya 4,000 walijitokeza mitaani huku wakikata kushiriki kwenye mazishi ya ndugu zao wakishinikiza serikali iwape majibu ya kina nani wameshiriki kwenye mauaji hayo.

Maelfu ya Waumini Washia wameandamana wakiwa wamebeba mabango yakionesha hasira waliyonayo kutokana na mauaji ya mara kwa mara ambayo yamekuwa yakiwalenga katika ardhi ya Pakistan.