AFRIKA KUSINI

Mwanaharakati Ramphele aanzisha Chama Cha Siasa kukabiliana na ANC kwenye uchaguzi ujao

Mwanaharakati Dr Mamphela Ramphele ambaye ameanzisha Chama Cha Siasa AGANG kupambana na ANC
Mwanaharakati Dr Mamphela Ramphele ambaye ameanzisha Chama Cha Siasa AGANG kupambana na ANC Reuters

Chama Tawala nchini Afrika Kusini cha ANC kimeendelea kupata upinzani kutokana na kuundwa kwa chama kipya kinachoongozwa na Mwanaharakati Mamphela Ramphele akiwa na lengo la kuleta mabadiliko.

Matangazo ya kibiashara

Chama kipya ambacho kimeundwa na Mwanaharakati Ramphele kinaitwa AGANG huku akiamini hicho ndiyo Chama ambacho kitaleta mabadiliko na kuwakomboa wananchi ambao wamekuwa kwenye makucha ya ANC kwa muda.

Mwanaharakati Ramphele amesema ANC ni Chama ambacho kimejawa na rushwa, ukabila na kuleana vitu ambacho vimechangia kwa kiasi kikubwa kushindwa kuendelea kwa taifa na wananchi wake.

Ramphela mwenye umri wa 65 akizindua Chama chake cha AGANG amewayaka wananchi wa Afrika Kusini kumuunga mkono na hatimaye kukiondoa madarakani Chama Cha ANC ambacho kinaonekana kushindwa kuwaletea maendeleo.

Mwanaharakati huyo mashuhuri nchini Afrika Kusini amesema maana ya jina AGANG ni “Tujenge” akiwa na maana huu ni wakati wa kujenga taifa hilo ambalo lina rasilimali nyingi na hazijawanufaisha wananchi wake.

Kiongozi huyo wa Chama Cha AGANG amesema kwa sasa wanatangaza vita dhidi ya rushwa kama ambavyo walifanya miaka 19 iliyopita wakati wakipambana na ubaguzi wa rangi kwenye nchi hiyo.

Makamu Mkuu huyo wa zamani wa Chuo Kikuu cha Cape Town amesema Taifa la Afrika Kusini lipo kwenye hatari ya watu kuweka mbele maslahi yao na tabia hiyo kama haitashughulikiwa kuna hatari juu ya mustakabali wa nchi.

Ramphele amesema Chama Cha AGANG kitashiriki kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi mkuu kitakachofanyika mwaka ujao wakiwa na lengo la kuking'oa madarakani Chama Cha ANC.

Mwanaharakati Ramphele amesema yupo tayari hata kuunda muungano ili kuhakikisha lengo lake ya kukiondoa madarakani ANC linatimia baada ya kuonekana ni Chama Cha nguvu lakini kwa sasa kimepoteza dira.