AFRIKA KUSINI

Mwendesha Mashtaka Nel asema Pistorius alimpiga risasi mpenzi wake Reeva kupitia mlango wa bafu

Mwanariadha Oscar Pistorius akiangua kilio mbele ya Mahakama ya Pretoria wakati shtaka lake linasikilizwa
Mwanariadha Oscar Pistorius akiangua kilio mbele ya Mahakama ya Pretoria wakati shtaka lake linasikilizwa

Mwendesha Mashtaka nchini Afrika Kusini ameanza kumuweka pabaya mwanaridha mwenye ulemavu wa miguu aliyeshinda medali ya dhahabu kwenye Olimpiki Oscar Pistorius baada ya kutoa ushahidi alimpiga risasi mpenzi wake Reeva Steenkamp akiwa bafuni. Mwendesha Mashtaka Gerrie Nel ameiambia Mahakama ya Pretoria iliyokuwa inasikiliza mchakato wa kuombwa kutoa dhamana kwa Mwanariadha huyo ya kwamba Pistorius alimpiga risasi mpenzi wake Reeva akiwa bafuni kupitia mlango wa bafu hilo.

Matangazo ya kibiashara

Hakimu anayesikiliza kesi hiyo Desmond Nair ameambiwa na Mwendesha Mashtaka Nel kuwa Pistorius alimpiga risasi mpenzi wake Reeva huku mwanamke huyo akiwa hajajihamu kwa silaha yoyote ambayo ingekuwa kitisho kwake.

Nel ameiambia Mahakama huko Pretoria ya kwamba Pistorius alimfyatulia risasi mpenzi wake Reeva akiwa umbali wa mita saba huku akitumia mlango wa bafu kurusha risasi nne zilizoingia mwilini kwa Mwanamitindo huyo.

Mwendesha Mashtaka Nel amemtaka hakimu Nair ambaye anasikiliza kesi hiyo kuridhia iwe ni kesi ya mauaji kutokana na namna ambavyo tukio hilo limetekelezwa na Pistorius dhidi ya mpenzi wake Reeva.

Mwanasheria wa Pistorius, Barry Roux ameendelea kusisitiza mbele ya Hakimu Nair ya kwamba mteja wake hakutenda kosa la mauaji kama ambavyo upande mashtaka umekuwa ukieleza na kutaka kosaliwe kuua bila kukusudia.

Roux amesema Mwendesha Mashtaka Nel ameshindwa kuonesha ushahidi wa dhati kwamba Pistorius ametenda kosa la mauaji kutokana na kukosa vithibitisho vya kutosha juu ya hilo.

Hakimu Nair alipomtaka Pistorius kujitetea akakosa neno la kueleza na kusalia kuitikia kwa muda wote huku akigugumia kwa kilio ambacho alikuwa anakitoa tangu mwanzo wa kusikilizwa kwa ombi la dhamana hadi mwisho.

Katika hatua nyingine Familia ya Mwanamitindo Reeva imefanya mazishi ya jamaa yao huku simanzi zikitawala kwenye shughuli hizo ambazo zimefanyika kwa usiri mkubwa huko Port Elizabeth.

Baba Mzazi wa Reeva, Barry Steenkamp baada ya kufanyika kwa mazishi hayo amesema mwanaye ataendelea kusalia kwenye mioyo yao siku zote kutokana na upekee aliokuwa nao kwenye maisha yake.

Naye kaka wa Marehemu Adam Steenkamp amesema pengo ambali limeachwa na Reeva hawezi kulifananisha na kitu chochote na wala hakuna mwanamke ambaye anaweza akajitokeza kuliziba.