MALI-UFARANSA-MAREKANI

Ufaransa yatangaza mpango wake wa kusaidia kuijenga upya Mali baada ya kukamilisha uvamizi wake wa Kijeshi

Serikali ya Ufaransa imetangaza kuwa tayari kujenga upya miundombinu nchini Mali baada ya kukamilika kwa vita
Serikali ya Ufaransa imetangaza kuwa tayari kujenga upya miundombinu nchini Mali baada ya kukamilika kwa vita REUTERS/Benoit Tessier

Serikali ya Ufaransa baada ya kuendesha mapambano ya kuyasambaratisha Makundi ya Kiislam Kaskazini mwa Mali hatimaye imeanza mpango wa kutoa misaada ya kimaendelea yenye nia ya kuijenga upya nchi hiyo iliyopita kwenye machafuko.

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa Maendeleo wa Ufaransa Pascal Canfin amesema baada ya kusitisha misaada yao jutokana na kufanyika kwa mapinduzi yasiyomwaga damu miezi kumi iliyopita wameamua kurejesha tena huduma hiyo kwa Mali.

Kauli ya Waziri Canfin ameitoa baada ya kutembelea Hospital iliyopo Mopti iliyojengwa kwa ushirikiano baina ya Ufaransa na Ubelgiji ambapo eneo hilo lilikuwa ni sehemu ya vita baina ya Jeshi la Mali na Wanamgambo wa Kiislam.

Waziri Canfin amesema jumla ya dola milioni 200 zitatolewa kwa Mali ili kuhakikisha shughuli zake za maendeleo zinakwenda na kuchangia kuijenga upya nchi hiyo hasa eneo la Kaskazini lililokuwa chini ya himaya ya Makundi ya Kiislam.

Kiongozi huyo katika serikali ya Ufaransa amesema wataelekeza juhudi zao hasa kwenye eneo la Timbuktu ambalo linapata huduma ya maji na umeme pekee hivyo watafanya kila linalowezekana kuhakikisha kila hitaji linapatika.

Umoja wa Ulaya EU nao kupitia Rais wa Tume ya Ulaya Jose Manuel Barroso umetangaza utayari wake wa kutoa msaada ikiwa ni pamoja na kuitisha mkutano wa nchi wahisani mwezi May kuisaidia Mali kujijenga upya.

Katika hatua nyingine serikali ya Marekani imetangaza utayari wake wa kushirikiana na Mali kijeshi lengo likiwa ni kudhibiti uwepo wa Makundi ya Kiislam yanayotajwa kuendesha vitendo vya kigaidi Kaskazini mwa Afrika.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ushirikino wa Kimataifa na Masuala ya Afrika Christopher Coons amesema kuna matumaini nchi yake itasaidia Mali moja kwa moja katika kuimarisha hali ya usalama.

Katika kufanikisha hilo Ujumbe wa Baraza la Seneti nchini marekani unatarajiwa kukutana na Rais wa Mpito wa Mali Dioncounda Traore, Ufaransa na Mawaziri wa Ulinzi wa nchi za Afrika kujadili hatua za kuchukua.

Ufaransa ndiyo nchi iliyoongoza uvamizi wa kijeshi Kaskazini mwa Mali kwa kushirikiana na Jeshi la Taifa hilo ambapo wakafanikiwa kuvunja ngome za Makundi ya Kiislam zilizokita mizizi kwa kipindi cha miezi tisa.