ZIMBABWE

ZANU-PF yataka vikwazo vyote dhidi ya Zimbabwe viondolewe na si vichache kama ambavyo Umoja wa Ulaya EU umefanya

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe akiwa na Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai
Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe akiwa na Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai REUTERS/Philimon Bulawayo

Chama Tawala nchini Zimbabwe ZANU-PF kimetaka vikwazo vyote ambavyo vimewekwa dhidi ya Taifa hilo viondolewe mara moja ili kutoa nafasi kwa nchi kuwexa kustawi zaidi kisiasa, kijamii na hata kiuchumi. Chama Cha ZANU-PF kimetoa tamko hilo ikiwa ni masaa kadhaa baada ya Umoja wa Ulaya EU kutangaza mpango wake wa kulegeza vikwazo ilivyokuwa imeviweka dhidi ya Zimbabwe kwa muda.

Matangazo ya kibiashara

Umoja wa Ulaya EU umefikia hatua ya kulegeza vikwazo hasa vile vya kusafiri na vya kibenki kutokana na kuridhishwa na mchakato wa mabadiliko ya kisiasa unaoendelea katika Taifa la Zimbabwe.

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wachama wa Umoja wa Ulaya EU ndiyo wamefikia makubaliano ya klegeza vikwazo dhidi ya Zimbabwe ambayo imekuwa ikikosolewa kutokana na namna inavyoendesha siasa zake.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza William Hague amesema wamefikia uamuzi wa kuodnoa baadhi ya vikwazo kutokana na Zimbabwe kupiga hatua hasa katika mchakato wa kupata katika mpya.

Hatua hiyo haijakiridhisha Chama Cha ZANU-PF kinachoongozwa na Rais Robert Gabriel Mugabe na badala yake wametaka vikwazo vyote vilivyowekwa dhidi yao viondolewe mara moja na mataifa hayo ya Magharibi.

ZANU-PF kimesema hatua hiyo bado haiwezi kusaidia ukuaji mwema wa Zimbabwe na badala yake juhudi zaidi zinapaswa kuchukuliwa na Umoja wa Ulaya EU katika kuondoa vikwazo hivyo.

Nacho Chama Cha Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai MDC kimepongeza hatua hiyo ya kulegezwa kwa vikwazo kulikofanywa na Umoja wa Ulaya EU na kuwataka Viongozi kuheshimu haki za binadamu.

Msemaji wa Chama Cha MDC Nelson Chamisa amesema wakati umefika kwa watu kuheshimu utawala wa sheria, haki za wananchi, kulinda kura na wapigakura pamoja na kuacha unyanyasaji dhidi ya wanaharakati.

Umoja wa Ulaya EU licha ya kulegeza vikwazo dhidi ya Zimbabwe lakini imesema vikwazo vingine vitaondolewa baada ya nchi hiyo kufanya uchaguzi wake na kama utakuwa na sura ya kidemokrasia taifa hilo litakuwa huru.