BULGARIA

Serikali ya Bulgaria yajiuzulu kutokana na kuendelea kwa maandamano ya kupinga Ubanaji wa Matumizi na Bei ya Umeme

Serikali nchini Bulgaria imetangaza kujiuzulu kutokana na kukerwa na muendelezo wa machafuko yaliyokuja baada ya kuibuka kwa maandamano yanayotaka kupunguzwa kwa bei ya umeme na kuondolewa kwa sera ya kubana matumizi. Waziri Mkuu wa Bulgaria Boyko Borisov ametangaza kujiuzulu kwa serikali yake kutokana na kuendelea kwa maandamano kwenye mitaa mbalimbali ya nchi hiyo yenye lengo la kuishinikiza serikali kuchukua hatua dhidi ya matakwa yao.

Waziri Mkuu wa Bulgaria Boyko Borisov ambaye ametangaza kujiuzulu kwa serikali yake
Waziri Mkuu wa Bulgaria Boyko Borisov ambaye ametangaza kujiuzulu kwa serikali yake REUTERS/Baz Ratner
Matangazo ya kibiashara

Maelfu ya wananchi wa Bulgaria wameonekana mitaani wakifanya maandamano kupinga kupanda kwa gharama za umeme sambamba na sera ya kubana matumizi iliyopendekezwa na serikali.

Waziri Mkuu Borisov amesema hawezi kuongoza nchi ambayo Jeshi la Polisi limekuwa mstari wa mbele kuwapiga wananchi wake wakati wakiwa wanadai haki zao za msingi kabisa.

Borisov ameliambia Bunge kutokana na vitendo hivyo vya ukatili vinavyofanywa na Jeshi la Polisi ameamua kuchukua hatua ya kujiuzulu yeye pamoja na serikali yake ili kupisha uongozi mwingine.

Kiongozi huyo wa Serikali amesema hawezi kuvumilia kuona vitendo vya uvunjaji wa sheria vikiendelea chini ya utawala wake ambao umeweka madarakani na hao wapigakura wanaonyanyaswa.

Borisov ameliambia Bunge ya kwamba wao wanaheshimu utu na hivyo hawawezi kuruhusu vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu vikaendelea kufanywa dhidi ya wananchi wenye dhamana kwenye utawala.

Jeshi la Polisi lilitumia nguvu kubwa kuwasambaratisha maelfu ya waandamanaji ambapo watu 25 walifikishwa hospital baada ya kurejuliwa vibaya kwenye mpambano huo baina yao na askari.