SYRIA

Umoja wa Mataifa UN watoa onyo hali ya Kibinadamu nchini Syria yazidi kuwa mbaya na misaada zaidi inahitajika

Mashambulizi yanayoendelea nchini Syria yamesababisha uharibifu pamoja na maelfu ya wananchi kuomba hifadhi wa ukimbizi katika nchi jirani
Mashambulizi yanayoendelea nchini Syria yamesababisha uharibifu pamoja na maelfu ya wananchi kuomba hifadhi wa ukimbizi katika nchi jirani REUTERS/Muzaffar Salman

Umoja wa Mataifa UN umetoa onyo kwamba kama hatua madhubuti hazitachukuliwa kuna kila dalili hali ya kibinadamu nchini Syria ikazidi kuwa mbaya zaidi kipindi hiki ambacho watu milioni nne wakihitaji msaada wa haraka. Tume ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Misaada ya Kibinadamu imeeleza hali imezidi kuwa mbaya kutokana na uwepo wa ongezeko la wakimbizi ambao wanakimbia Syria kutokana na kuendelea kwa mapigano.

Matangazo ya kibiashara

Mkuu wa Tume hiyo Valerie Amos ametaka hatua za haraka zichukuliwe katika kukabiliana na tatizo hilo la ukosefu wa huduma muhimu za kibinadamu dhidi ya wananchi ambao wanashuhudiamapigano yakizidi kusonga mbele.

Amos amesema hakuna kificho cha yale ambayo yanaendelea nchini Syria kwani kila mmoja anayaona kwa macho yake hivyo yapaswa kuchukua hatua za haraka katika kuwasaidia wananchi wanaohitaji msaada.

Mkuu huyo wa Tume ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Misaada ya Kibinadamu limeelekeza lawama zake kwa serikali ya Damascus kutokana na kukataa kuruhusu misafara ya misaada kuingia ikitokea Uturuki.

Amos ameitaka Jumuiya ya Kimataifa kuchukua hatua za haraka kuwasiadia wakimbizi wa Syria walio katika nchi za jirani ambao wameomba hifadhi baada kushuhudia vita vinavyokaribia miezi ishirini na nne sasa.

Hayo yanakuja kipindi hiki ambacho mapigano yamezidi kushika kasi ambapo idadi ya watu waliopoteza maisha katika shambulizi la roketi huko Jijini Aleppo ikifika watu 33 na hivyo kuongeza hofu ya usalama.

Mashambulizi yameendelea kushuhudiwa huku wapinzani wakiendelea kupambana na wanajeshi watiifu kwa serikali ya Rais Bashar Al Assad na taarifa zinasema makazi ya Kiongozi huyo yameanza kulengwa.

Wapiganaji wa Upinzani wamefanya mashambulizi ambayo yamelenga moja ya kasri la Rais Assad ambalo analitumia kama makazi yake kitu ambacho kinatajwa kama ishara ya kuendelea kwa mapigano hayo kwa muda mrefu.

Mashambulizi haya yanatokea siku moja baada ya Rais Assad kutangaza kwamba wanajeshi wake watashinda kwenye vita inayoendelea na kugharimu maisha ya zaidi ya watu 60,000 na kudumu kwa miezi 23 dhidi ya vibaraka.