UGIRIKI

Jeshi la Polisi nchini Ugiriki lakabiliana vilivyo na Waandamanaji wanaopinga Ubanaji wa Matumizi Jijini Athens

Jeshi la Polisi nchini Ugiriki katika Jiji la Athens wamekuwa na kibarua kizito cha kukabiliana na Waandamanaji waliojitokeza kwenye mitaa mbalimbali wakipinga mpango wa serikali wa kubana matumizi.

Wafanyakazi nchini Ugiriki wakiwa kwenye maandamano mitaani kupinga sera ya ubanaji wa matumizi
Wafanyakazi nchini Ugiriki wakiwa kwenye maandamano mitaani kupinga sera ya ubanaji wa matumizi REUTERS/Costas Baltas
Matangazo ya kibiashara

Maandamano hayo yalikuwa ni matokeo ya mgomo wa kwanza kufanyika nchini Ugiriki kwa mwaka huu ambapo wafanyakazi walijitokeza mitaani kuendelea kutoa kilio chao wakitaka serikali iachane na mpango wa kubana matumizi.

Watu wapatao 15,000 ambao ni wafanyakazi walishiriki kwenye mgomo ulioandaliwa na Jumuiya mbalimbali katika Jiji la Athens huku wengine 20,000 wakishiriki kwenye maandamano yaliyoandaliwa na Vyama vya Wafanyakazi.

Jeshi la Polisi limesema licha ya maandamano hayo yaliyofanyika Jijini Athens lakini watu wengine 15,000 walijitokeza mitaani Kaskazini mwa Ugiriki katika Mji wa Thessaloniki wakiishinikiza serikali kuachana na kubana na matumizi.

Waandamanaji hao wakiwa wamejihami na mabomu ya petroli sambamba na mawe walikuwa wakipambana na askari ambao walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwasambaratisha.

Maandamano hayo yamechangia hasra kubwa kutokana na waandamanaji kushambulia maduka pamoja na kuharibu magari mengi ambayo yalikiwepo wakati wakiendelea na mapambano yao dhidi ya Polisi.

Wengi wa waandamanaji wamesema hawataki mpango wa kubana matumizi kwa kuwa ni chanzo cha kufukuzwa kazi kwa wafanyakazi wengi na hivyo wengi huenda wakaangukia kwenye lindi la umasikini.

Mwenyekiti wa Umoja wa Sekta Binafsi nchini Ugiriki GSEE Yiannis Panagopoulos amesema wafanyakazi na wananchi wataendelea kupigania haki zao kutokana na sera ya kubana matumizi kuwa hatari kwao.

Panagopoulos amesema umoja ambao umekuwa ukioneshwa na wananchi unapaswa kuendelezwa kwa manufaa yao kwani sera hiyo ya kubana matumizi ikipata mashiko wengi sana wataathirika.

Ugiriki ilionekana kuanza mwaka 2013 kwa utulivu bila ya uwepo wa maandamano na migomo kama iliyoshuhudiwa mwishoni mwa mwaka jana na tukio hili limeanza kuleta hofu upya.