MALAWI

Serikali ya Malawi yatangaza haina uwezo wa kuongeza mshahara kwa wafanyakazi na kuomba migomo kusitishwa

Wafanyakazi nchini Malawi wakiwa kwenye maandamano kushinikiza nyongeza ya mshahara kwa serikali
Wafanyakazi nchini Malawi wakiwa kwenye maandamano kushinikiza nyongeza ya mshahara kwa serikali

Serikali nchini Malawi imesema haiwezi kuongeza mshahara kwa wafanyakazi wake kwa sasa licha ya wafanyakazi wa umma kufanya mgomo mkubwa ambao umeathiri safari za ndege na shughuli nyingine za kiuchumi.

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa Fedha wa Malawi Ken Lipenga amesema licha ya kuendelea kwa mgomo na maandamano ya wafanyakazi lakini serikali kwa sasa haiwezi kumudu kuongeza mishahara kwa wafanyakazi wake wa umma.

Waziri Lipenga amesema kwa mujibu wa matumizi ya serikali yaliyopangwa haiwesekani kwa sasa wakaongeza msharaka kwani bajeti waliyonayo haitoshi kufanya mabadiliko ya aina yoyote ile.

Lipenga amewataka wafanyakazi kuwa watulivu kwani kwa sasa serikali haina uwezo tena wa kuongeza mishahara na hivyo wametaka kupatiwa muda zaidi ili waweze kushughulikia mapendekezo hayo.

Wafanyakazi wa kwenye Viwanja vya Ndege nchini Malawi wamefanya mgomo mkubwa ambao umechangia kusitishwa kwa safari za ndani na nje ya Taifa hilo kutokana na wao kuwa kwenye maandamano ya kusaka malipo bora.

Safari zote zimelazimika kusitishwa nchini Malawi huku wafanyakazi hao wakifanya maandamano yao kwenye Jiji la Blantyre wakiitaka serikali kuongeza mshahara kwa wafanyakazi nchini humo.

Mgomo huo haukuishia kwenye Viwanja vya ndege pekee bali uligusa sekta nyingine na kuchangia kukwama kwa shughuli za serikali kutokana na wafanyakazi kuweka zana zao chini na kuitaka serikali kusikiliza kilio chao cha kulipwa mshahara mdogo.

Mgomo huo unatajwa kuwa mkubwa zaidi kufanyika nchini Malawi ikiwa chini ya uongozi wa Rais Joyce Banda ambaye anatarajiwa leo kuelekea nchini Equatorial Guinea kwa ajili ya ziara ya kikazi.

Haijabainika hadi sasa iwapo Rais Banda anaweza kuendelea na safari yake kutokana na Viwanja vikubwa vya ndege vya Lilongwe na Blantyre navyo kukutwa na mgomo huo na kushindwa kuendesha shughuli zake.

Wafanyakazi wanaokadiri wa kufikia 120,000 wameshiirki kwenye mgomo huo wakiwemo waalimu na maofisa wa uhamiaji ambao wanaitaka serikali kuhakikisha wanafanyaka kila linalowezekana ili kuongeza mshahara.

Wafanyakazi hao wamesema tangu serikali ya Rais Banda ilipokubali kushusha thamani ya fedha yao ya kwacha kwa asilimia 49 mwezi May ndiyo imechangia hali ya maisha kuwa ngumu na mshahara unaopatikana hautoshi.