SYRIA-URUSI

Urusi na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu zataka mazungumzo ya ana kwa ana baina ya Serikali ya Syria na Upinzani

Jiji la Aleppo linavyoonekana baada ya machafuko ya miezi 23 nchini Syria baina Serikali na Upinzani
Jiji la Aleppo linavyoonekana baada ya machafuko ya miezi 23 nchini Syria baina Serikali na Upinzani

Serikali ya Urusi na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu zimesema zinahitaji kufanyika kwa mazungumzo ya ana kwa ana kati ya Serikali ya Syria na Viongozi wa Upinzani lengo likiwa ni kumaliza umwagaji wa damu unaoendelea kwa miezi karibu 24 sasa. Waziri wa Mambo ya Nje Sergei Lavrov amesema machafuko yanayoendelea katika ardhi ya Syria hayawezi kuleta suluhu ya aina yoyote na badala yake hatima ya baadaye ya nchi hiyo inaharibika kutokana na hali hiyo kuendelea.

Matangazo ya kibiashara

Pendekezo la Urusi na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu limekuja huku Baraza la Muungano la Upinzani nchini Syria likijiandaa kuanza mkutano wake wa siku mbili nchini Misri kujadili njia ambazo zinaweza zikasaidia kupatikana kwa suluhu.

Waziri Lavrov amesema pendekezo lao limekuja baada ya kufanya mazungumzo na Viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na kukubaliana njia pekee ni kushawishi yafanyike mazungumzo ya ana kwa ana kati ya serikali na upinzani.

Kauli ya serikali ya Urusi imekuja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje Lavrov kukutana na Mawaziri wengine wa Mambo ya Nje kutoka Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ambao wamekuwa wakiituhumu Moscow kuisaidia serikali ya rais Bashar Al Assad.

Urusi imesema haifutahishwi na mauaji yanayoendelea kufanyika nchini Syria lakini pia haiungi mkono mpango wa Mataifa ya Magharibi ya kutaka Utawala wa Rais Assad uondolewe madarakani na badala yake nnjia ya diplomasia inafaa zaidi.

Waziri Lavrov na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Nabil El Araby kwa kauli moja wamesema kipaumbele chao ni kuhakikisha serikali ya mpito inatengenezwa ili kuhakikisha machafuko yanadhibitiwa kabisa.

Mapngo huu wa Urusi na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu umeanza kupata upinzani kutoka kwa Baraza la Upinzani nchini Syria ambapo mmoja wa Kiongozi wake Abdelbaset Sieda amesema wao wanataka utawala uliopo madarakani ukae kando.

Takwimu zinaonesha karibu watu 70,000 wamepoteza maisha katika kipindi cha miezi 23 ya machafuko yanayoendelea nchini Syria yakiwa na lengo la kuuangusha Utawala wa Rais Bashar Al Assad.