SYRIA

Watu 31 wapoteza maisha nchini Syria baada ya bomu lililotegwa kwenye gari kulipuka katika Jiji la Damascus

Shambulizi la kujitoa mhanga lililotekelezwa nchini Syria limesababisha watu 31 kupoteza maisha baada ya bomu lililokuwa limetegwa kwenye gari kulipuka katika Jiji la Damascus karibu na Makao makuu ya Chama cha Baath. Mashirika ya Kutetea Haki za Binadamu yamethibitisha kutokea kwa mashambulizi manne tofauti nchini Syria katika Jiji la Damascus yanayotajwa kutekelezwa na Wapiganaji wa Upinzani.

Shambulizi la Bomu la Kujitoa Mhanga lililotekelezwa Jiji Damacus na kusababisha vifo vya watu 31
Shambulizi la Bomu la Kujitoa Mhanga lililotekelezwa Jiji Damacus na kusababisha vifo vya watu 31
Matangazo ya kibiashara

Wengi wa waliopoteza maisha kati ya hao 31 ni raia wa kawaida ambapo taarifa zinasema watu wengine wengi wamejeruhiwa bila ya kutajwa idadi kamili ya wale waliopata majeraha kwenye mashambilizi hayo.

Shambulizi la bomu la kujitoa mhanga lililotekelezwa kwenye Makao Makuu ya Chama tawala Cha Baath ndilo linatajwa kuchangia vifo vya watu wengi zaidi huku mashambulizi mengine yakifanywa katika eneo la Mazraa.

Televisheni ya taifa inayounga mkono serikali ya Rais Bashar Al Assad imesema mashambulizi hayo ni muendelezo wa mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na wapinzani wa serikali.

Televisheni ya Al-Ikhbariya imeonesha baadhi ya video za shambulizi hilo huku watu wengi wakionekana kuhaha huku na kule katika kuwaokoa manusura wa shambulizi hilo katika Jiji la Damascus.

Kwa mujibu wa Televisheni ya Al-Ikhbariya miongoni mwa waliopoteza maisha ni pamoja na watoto wanne waliokuwa karibu kabisa na Makao Makuu ya Chama Tawala cha Baath huku wengine wakijeruhiwa.

Mashuhuda wa shambulizi hilo wamesema waliona gari moja likilipuka kwenye kituo cha ukaguzi wa magari kilichopo karibu na Ubalozi wa Urusi na Makao Makuu ya Chama Tawala Cha Baath.

Jiji la Damascus limeimarishiwa ulinzi zaidi katika siku za hivi karibuni kwa kuweka vituo vingi vya ukaguzi wa magari lakini bado kumekuwa na mashambulizi ya kujitoa mhanga yanayotekelezwa.

Shambulizi hili linakuja huku Urusi na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu zikipendekeza kufanyika kwa mazungumzo ya ana kwa ana kati ya serilali ya Damascus na Baraza la Taifa la Upinzani.

Kwa upande wake upinzani unaendelea na mkutano wao wa siku mbili ulioanaza hii leo nchini Misri kuangalia namga ya kupata suluhu ya umwagaji wa damu uliodumu kwa karibu miezi 24.

Takwimu za hivi karibuni zinakadiria watu 70,000 wamepoteza maisha tangu kuanza kwa machafuko nchini Syria mwezi Machi mwaka 2011 ambapo upinzani umekuwa ukipambana na serikali ya rais Assad.