SYRIA

Damascus yakumbwa na shambulizi baya zaidi tangu kuanza kwa vita vilivyodumu kwa miezi 24 sasa

Shambulizi mbaya zaidi kutokea nchini Syria katika Mji Mkuu Damascus tangu kuanza kwa vita karibu miezi 24 limesababisha vifo vya watu wanaokadiriwa kufikia 60 na kuongeza hofu ya usalama katika nchi hiyo.

Mabaki ya magari yaliyosababishwa na mlipuko wa bomu uliotekelezwa katika Jiji la Damascus, Syria
Mabaki ya magari yaliyosababishwa na mlipuko wa bomu uliotekelezwa katika Jiji la Damascus, Syria REUTERS
Matangazo ya kibiashara

Shambulizi hilo la bomu la kujitoa mhanga lililotekelezwa kwa kutumia gari limelaaniwa na pande zote ule wa serikali na upinzani ya kwamba limefanywa na magaidi wasioitakia mema Syria.

Bomu hilo la kujitoa mhanga limetekelezwa karibu na Makao Makuu ya Jeshi na kuonesha lilikuwa linalenga kuchukua uhai wa Viongozi wa Jeshi wanaomtii Rais Bashar Al Assad ambaye anakabilia na upinzani kwa miezi 24 na sasa.

Televisheni ya Taifa nchini Syria imeonesha picha za tukio hilo huku watu wengi wakionekana kuhaha kunusuru maisha yao pamoja na kubeba miili ya watu waliopoteza maisha.

Mashirika ya Kutetea Haki za Binadamu nchini Syria yamethibitsha watu 59 wamepoteza maisha wakiwemo wanajeshi 15 huku watu wengine zaidi ya 200 wakijeruhiwa vibaya kwenye shambulizi hilo.

Hili ni shambulizi baya zaidi kutoka katika Jiji la Damascus tangu watu 55 kupoteza maisha tarehe 10 mwezi May mwaka 2012 ambapo mashambulizi mawili ya kujitoa mhanga walitikisa Jiji hilo.

Shambulizi hilo limetekelezwa huku Baraza la Upinzani nchini Syria likiendelea na mkutano wake nchini Misri kupendekeza njia muafaka ambazo zitasaidia kumaliza umwagaji wa damu uliosababisha vifo vya watu karibu 70,000.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon amelaani vikali shambulizi hilo ambalo amesema limeendelea kugharimu maisha ya wananchi wasio na hatia na hivyo kuzitaka pande zote kuacha mashambulizi.

Ban amesema kutokana na mauaji yanayoendelea kushuhudiwa ni bora pande zinazohasimiana nchini Syria kuweka silaha chini na kutumia njia mbadala katika kushughulikia umwagaji wa damu unaoendelea.