VENEZUELA

Kamanda Hugo Chavez aendelea kusumbuliwa na maradhi ya kupumua akipoa upasuaji wa saratani aliyofanyiwa Cuba

Rais wa Venezuela Kamanda Hugo Chavez ambaye amerejea nyumbani mapema juma hili anaendelea kukabiliwa na matatizo ya kupumua kitu ambacho kinatajwa huenda kikawa kikwazo kwake kuweza kupona haraka na kurejea kwenye shughuli zake.

Rais wa Venezuela Hugo Chavez akiwa na binti zake wawili Hospital akiendelea kupatiwa matibabu
Rais wa Venezuela Hugo Chavez akiwa na binti zake wawili Hospital akiendelea kupatiwa matibabu REUTERS/Ministry of Information/Handout
Matangazo ya kibiashara

Waziri wa Habari Ernesto Villegas ndiye ametoa taarifa hiyo na kusema Kamanda Chavez ameendelea kusumbuliwa na tatizo la kupumua ambalo lilimuanza baada ya kufanyiwa upasuaji wa saratani nchini Cuba.

Villegas amesema tatizo hilo la upumuaji ndilo ambalo limekuwa kikwazo kwa sasa kwa Rais Chavez kuweza kurejea kwenye shughuli zake na hivyo analazimika kuendelea kupata matibabu kwenye Hospital ya Kijeshi.

Jopo la Madaktari linaendelea kutoa matibabu kwa Rais Chavez ili kuhakikisha wanalidhibiti tatizo la kupumua ambalo linamkabili kwa sasa huku upasuaji wa saratani inayomsumbua kidonda chake kikiendelea vizuri.

Kamnda Chavez mwenye umri wa miaka 58 na amekuwa madarakani tangu mwaka 1999 ameendelea kuwasiliana na ndugu wa karibu na Viongozi wa serikali ambao amekuwa akiwapa maelezo ya kuendesha serikali.

Villegas amesema wanauhakika Madaktari wanaomtibu Kamanda Chavez watafanikiwa kulimaliza tatizo la kupumua linalomkabili Kiongozi huyo aliyeshinda kwenye uchaguzi mkuu hapo mwaka jana.

Hizi ni taarifa za kwanza kutolewa hadharani tangu kurejea nyumbani ghafla kwa Kamanda Chavez aliyekuwa nchini Cuba kwa kipindi cha zaidi ya miezi miwili akipatiwa matibabu ya saratani na kufanyiwa upasuaji mara nne.

Serikali ya Caracas haijawahi kueleza wazi ni saratani ya aina gani inayomsumbua Rais Chavez huku Makamu wa Rais Nicolas Maduro akisema kila kitu kitaendelea kama kilivyopangwa licha ya Kiongozi wao kusumbuliwa na maradhi.

Tangu arejee nyumbani Rais Chavez na kutangaza kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter ametembelea na Rais wa Bolivia Evo Morales ambaye hata hivyo hakuruhusiwa kumuona na badala yake akazungumza na Madaktari pamoja na ndugu wa karibu wa Chavez.