KENYA-UCHAGUZI

Wananchi wa Kenya wahakikishiwa usalama wakati wa uchaguzi mkuu

Tume Huru ya Uchaguzi na Ukaguzi wa Mipaka nchini Kenya IEBC imetangaza ipo tayari kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaofanyika hapo kesho na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi na kisha kurejea nyumbani kusubiri matokeo yatakayotangazwa. Mwenyekiti wa IEBC Ahmed Isaack Hassan amejitokeza kwa mara ya mwisho mbele ya wanahabari kwenye kituo kitakachotumika kujumlishia na kutangazia matokeo ya mwisho ya uchaguzi na kueleza siku tatu pekee zinatosha kumtangaza mshindi.

in2eastafrica.net
Matangazo ya kibiashara

Hassan amesema watatoa kipaumbele cha kwanza kwa matokeo ya urais ambayo yatatangazwa mapema tofauti na siku saba kama ambavyo katiba ya Jamhuri ya Kenya inavyotaka.

Hassan amewaondoa hofu Makamishna wa Tume yake kwa kueleza wameIshafanya mawasiliano na Jeshi la Polisi ambalo litashika doria kipindi chote cha uchaguzi huo.

Kwa upande wake Jeshi la polisi limesema kuwa mikakati yote ya kiusalama imekamilika na wale watakaojaribu kuvuruga zoezi hilo watadhibitiwa haraka iwezekanavyo.

Masaa kadhaa pekee ndio yamesalia kabla ya kufunguliwa kwa vituo vya kupigia kura ambapo wapiga kura milioni kumi na nne wanatarajiwa kutumia haki yao ya kikatiba kuwachagua viongozi wa serikali ya wamu ya nne.