KENYA-UCHAGUZI

Muungano wa CORD wataka uhesabuji wa kura za Urais usitishwe

REUTERS/Thomas Mukoya

Mgombea mweza wa Waziri Mkuu Raila Odinga, na Makamu wa Rais anayemaliza muda wake Kalonzo Musyoka ametoa wito kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya nchini Kenya IEBC kusitisha zoezi la kuhesabu kura za Urais baada ya kubainika kwa kasoro katika baadhi ya maeneo.

Matangazo ya kibiashara

Musyoka kutoka muungano wa kisiasa wa CORD amesema wana uthibitisho kuwa kumekuwa na udanganyifu katika zoezi hilo kwani katika baadhi ya maeneo kura za jumla zimekuwa zikizidi idadi ya wapiga kura waliojisajili hapo awali.

Licha ya kutoa kauli hiyo, Musyoka amewataka wananchi wa Kenya kuwa watulivu wakati huu kwani tuhuma hizo alizozitoa hazina lengo la kuhimiza maandamano ama vurugu kwani muungano wao unajiendesha kwa misingi ya sheria.

Maswali kadhaa yameendelea kuibuka baada ya mfumo wa uhesabuji kura wa kielekroniki wa IEBC kupata hitilafu na kulazimika zoezi la uhesabuji wa kura kuanza upya kwa njia ya kawaida.

Wakati hayo yanajiri IEBC imekuwa ikiendelea na uhesabuji wa kura hizo za Urais na imesema itatoa matokeo ya mwisho ifikapo siku ya Ijumaa asubuhi.

Licha ya IEBC kushindwa kutoa matokeo ndani ya saa arobaini na nane kama ilivyoahidi hapo awali kumekuwa na utulivu wakati wananchi wakiendelea kusubiri kinachoendelea kutoka Ukumbi wa Bomas jijini Nairobi ambapo matokeo rasmi yanaendelea kutolewa.

Kwa matokeo ya hivi sasa mgombea urais kwa tiketi ya muungano wa Jubilee Uhuru Kenyatta anaongoza akifuatiwa na Waziri Mkuu Raila Odinga ambaye ni mgombea wa muungano wa CORD.