KENYA

Uhuru Kenyatta atangazwa rasmi kinara wa kiti cha urais wa Kenya

Tume huru ya uchaguzi na ukaguzi wa mipaka ya nchini Kenya IEBC imemtangaza rasmi Uhuru Kenyata kuwa mshindi wa kiti cha uraisi ikiwa ni baada ya kukamilika kwa zoezi la kuhesabu kura kutoka katika maeneo yote nchini humo.

Rais mteule wa Kenya Uhuru Muigai Kenyatta
Rais mteule wa Kenya Uhuru Muigai Kenyatta rfi
Matangazo ya kibiashara

 

Tume hiyo imemtangaza uhuru baada ya matokeo hayo kuthibitishwa na kupitishwa na maafisa wa tume hiyo.

Kenyatta amepata asilimia 50.07 ya kura zote zilizopigwa huku mpinzani wake wa karibu Raila Odinga akipata asilimia 44.

Odinga aliyeangushwa katika kinyang'anyiro hicho amesema watakwenda mahakamani kupinga matokeo hayo baada ya IEBC kufanya makosa katika utendaji wake na wana uthibitisho wa udanganyifu uliofanywa katika baadhi ya maeneo.

Waziri Mkuu huyo anayemaliza muda wake ameshindwa kutwaa nafasi hiyo kwa mara ya tatu sasa lakini atakumbukwa sana katika harakati zake za kupigania upatikanaji wa katiba mpya na kuhimiza utawala bora nchini humo.

Wakati huo huo vifijo na nderemo vimetawala katika maeneo mbalimbali nchini humo ambapo wafuasi wa Muungano wa Jubilee wamejitokeza kushangilia ushindi huo.

Rais mteule Kenyatta ana kesi ya kujibu katika Mahakama ya Kimataifa ya ICC anakotuhumiwa kuchochea na kufadhili machafuko ya baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 na kesi yake imesogezwa mbele na mahakama hiyo mpaka mwezi Julai mwaka huu.

William Ruto ambaye alikuwa mgombea mwenza wa Kenyatta naye pia anakabiliwa na mashtaka katika Mahakama ya ICC, akituhumiwa kuhusika na machafuko hayo yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu elfu moja na maelfu kupoteza makwao.