KENYA-CHINA

China yapongeza ushindi wa Rais mteule wa Kenya Uhuru Muigai Kenyatta

Mataifa mbalimbali yameendelea kutuma salamu za pongezi kwa Rais mteule wa Kenya, Uhuru Muigai Kenyatta ambaye aliibuka kinara wa kiti cha urais wa nchi hiyo baada ya kupata ushindi wa asilimia 50.07 dhidi ya asilimia 44 za mpinzani wake wa karibu Raila Amolo Odinga.

rfi
Matangazo ya kibiashara

Jumatatu hii wizara ya mambo ya nje ya China imetuma salamu za pongezi kwa Kenyatta ambaye anakabiliwa na mashtaka katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC ya The Hague.

Msemaji wa wizara hiyo Hua Chunying amewaambia waandishi wa habari kuwa wanampongeza Kenyatta kwa ushindi huo na pia wanalipongeza Taifa la Kenya kwa kuendesha zoezi hilo kwa amani na utulivu.

Kenyatta ameweka historia ya kuwa mtu wa kwanza kushinda kiti cha urais wakati akikabiliwa na mashataka katika mahakama ya ICC.

Hata hivyo ushindi wake umepingwa na muungano wa kisiasa wa CORD ambao umesema utatinga mahakamani jumatatu hii kutaka hatua za kisheria dhidi ya udanganyifu uliofanywa katika baadhi ya maeneo.

Hapo jana jumapili muungano wa CORD uliteua mawakili 10 ambao watawawakilisha katika mahakama ya juu kuhakikisha haki inatendeka.

Iwapo mahakama itabaini kuwa kulikuwa na dosari katika uchaguzi huo itatoa uamuzi wa kufanyika kwa uchaguzi mwingine ndani ya siku sitini na iwapo hakutakuwa na dosari yoyote Rais mteule Kenyatta na Naibu wake Wiliam Ruto wataapishwa mwezi Aprili mwaka huu.