KENYA-ICC

ICC yamuondolea mashtaka aliyekuwa Mkuu wa utumishi wa umma wakati wa machafuko ya kisiasa nchini Kenya

Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu ya ICC imemwondolea mashtaka yote yanayomkabili aliyekuwa Mkuu wa utumishi wa Umma nchini Kenya Francis Muthaura baada ya upande wa Mashtaka kusema kuwa kwa sasa hawana ushahidi wa kutosha dhidi ya Muthaura kama alijihusisha na kuchochea na kufadhili ghasia za nchini Kenya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.

Matangazo ya kibiashara

Kiongozi wa Mashtaka Fatoue Bensuda amesema ushahidi alionao kwa sasa hautoshi kumshIitaki Muthaura kwa kile alichokisema baadhi ya mashahidi tayari wamekufa na wengine wamekataa kushirkiana na upande wa mashataka.

Aidha Bensouda amesema serikali ya Kenya haijaonyesha ushirikiano wa kutosha na ameelezwa kusikitishwa kwake baada ya serikali hiyo kushindwa kuwasilisha vielelezo muhimu kuhusiana na kesi hiyo.

Muthaura amekuwa akishtakiwa katika mahakama ya ICC sambamba na Rais mteule Uhuru Muigai Kenyatta na Naibu wake William Ruto ambao kesi yao ilisogezwa mpaka mwezi julai ili kupisha shughuli za uchaguzi mkuu wa Taifa la Kenya.

Watu zaidi ya elfu moja waliuawa katika machafuko yaliyolikumba Taifa hilo baada ya upinzani kupinga matokeo ya uchaguzi huo yaliyomtangaza Mwai Kibaki kuwa mshindi katika kinyanganyiro cha Urais dhidi ya Waziri Mkuu anayemaliza muda wake hivi sasa Raila Odinga.