ITALIA

Mchakato wa kumtafuta Papa wa kanisa katoliki waingia siku ya pili

dailymail.co.uk

Mchakato wa kumpata kiongozi mpya wa juu wa kanisa katoliki unaoendelea katika makuu ya Kanisa hilo mjini Vatican nchini Italia bado haujazaa matunda baada ya Makadinali 115 wa Kanisa hilo duniani kote kushindwa kumchagua Papa mpya katika siku ya kwanza ya zoezi la upigaji kura.

Matangazo ya kibiashara

Moshi mweusi ulionekana ikiwa na maana kuwa Makadinali hao bado hawajafanikiwa kumpata kiongozi wao na leo hii wanatarajiwa kupiga kura mara nne.

Macho na masikio ya waumini wa kanisa hilo duniani kote bado yameelekezwa mjini Vatican kusubiri kutoka kwa moshi mweupe ambao ni ishara ya kupatikana kwa Papa mpya.

Papa atakayepatikana atakuwa anaziba pengo lililoachwa na Papa Benedicto wa 16 ambaye sasa anafahamika kama Papa Emeritus aliyejiuzulu mwezi uliopita kwa sababu za umri mkubwa na matatizo ya kiafya.

Kiongozi huyo atakuwa na jukumu la kuongoza takribani waumini bilioni moja nukta mbili wa kanisa hilo duniani kote na atakuwa Papa wa 266 katika historia ya kanisa hilo.