ITALIA

Kadinali Jorge Mario Bergoglio wa Argentina ndiye Papa mpya wa kanisa katoliki

REUTERS/Alessandro Bianchi

Kadinali Jorge Mario Bergoglio mwenye umri wa miaka sabini na sita kutoka Argetina ndiye kiongozi mpya wa kanisa katoliki duniani. Kiongozi huyo sasa atakujalikana kama Papa Francis wa kwanza na baada ya kuchaguliwa katika makao makuu ya kanisa hilo mjini Vatican nchini Italia amezungumza kwa mara ya kwanza na waumini wa kanisa hilo.

Matangazo ya kibiashara

Papa huyo mpya hakuwa anapewa nafasi kubwa ya kuibuka mshindi katika uchaguzi huo na baada ya kuchaguliwa aliwashukuru Makadinali kwa kumpa nafasi na kuwasihi waumini wa kanisa hilo kumuombea ili aweze kutimiza majukumu yanayomkabili.

Papa Francis wa Kwanza anachuakua nafasi ya Papa Benedicto wa kumi na sita aliyejizulu mwezi uliopita na anachukua uongozi wa kanisa hilo wakati ambapo linakabiliwa na changamoto za nafasi ya wanawake pamoja na kuwaunganaisha zaidi ya waumini bilioni mbili wa kanisa hilo duniani kote.

Papa Francis wa kwanza anawaongoza makadinali katika misa yake ya kwanza leo alhamisi katika makao makuu ya kanisa katoliki duniani mjini Vatican ikiwa ni misa ya kwanza kwake kuongoza tangu apate wadhifa huo.

Misa ya kusimikwa rasmi Papa Francis wa kwanza inatarajiwa kufanyika tarehe 19 ya mwezi huu.

Viongozi mbalimbali duniani wamekuwa wakituma salamu za pongezi kwa Papa Francis wa kwanza huku wakimtaka kuzingatia maswala ya amani, usawa na haki za binadamu.