RWANDA

Rwanda yakanusha kuwepo kwa waasi wa M 23 nchini humo

Serikali ya Rwanda kupitia Waziri wa mambo ya nje Louise Mushikiwabo imetupilia mbali madai ya serikali ya DRC kuwa Jenerali Bosco Ntaganda anayesakwa na Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu wa kivta ICC amevuka mpaka na kuingia Rwanda.

Matangazo ya kibiashara

Itakumbukwa kuwa mwishoni mwa juma lililopita, wapiganaji wapatao 700 wa M 23 wa upande wa Jean- Marie Runiga walivuka mpaka kukimbilia nchini Rwanda baada ya makabiliano makali na upande wa M23 wanaoongozwa na Sultan Makenga.

Hata hivyo, serikali ya DRC kupitia msemaji wake Lambert Mende inaomba nchi ya Rwanda kuwapeleka mbele ya vyombo vya sheria vya kimataifa wale ambao wanatafutwa kwa makosa ya uhalifu wa kivita.

Mashirika ya kiraia katika Jimbo la Kivu ya Kaskazini kwa upande wao, yametoa msimamo wao kuhusiana na taarifa hizo, huku Omar Kavota naibu Mwenyekiti na msemaji wa mashirika hayo akisema viongozi hao wa M 23 wameitwa Rwanda na viongozi wa serikali hiyo.

Rwanda imeendelea kushtumiwa na Umoja wa Mataifa kwa kuwaunga mkono waasi hao kwa kuwahami kwa silaha madai ambayo serikali ya Kigali imeendelea kukanusha.

Ukosefu wa usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokarasia ya Congo umesababisha zaidi ya watu elfu 20 kukimbia makwao wengi wakitafuta makao nchini Rwanda na Uganda.

Mgawanyiko kati ya waasi wa M 23 kati ya kundi la  Jean Marie Runinga na Betrand Bissimwa umekwamisha kusainiwa kwa mkataba wa maelewano kati ya serikali ya Kinsasha na waasi hao wa M 23  jijini Kampala Uganda huku kila kundi likidai kuwa ndilo halali.