SOMALIA

Shambulizi la bomu mjini Mogadishu lasababisha maafa ya watu wanane

Watu wanane wameuawa mjini Mogadishu nchini Somalia baada ya kutokea kwa shambulizi la bomu la kujitoa mhanga siku ya Jumatatu.

Matangazo ya kibiashara

Mohamed Duale afisa wa Polisi mjini huo amethibitisha kutokea kwa shambulizi hilo baada ya bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari ndogo kulipuka karibu na Ofisi ya kitaifa ya sanaa.

Hadi sasa hakuna kundi lililojitokeza kudai kuwa limetekeleza shambulizi hilo lakini inashukiwa kuwa kundi la kigaidi la Al-Shabab ambalo limekuwa likitekeleza mashambulizi kama hayo mara kwa mara linahusika.

Idadi kubwa ya watu waliopoteza maisha yao walikuwa ndani ya basi ndogo lililolengwa na shamabulizi hilo baada ya kutokea kwa mlipuko mkubwa.

Wanamgambo wa Al-Shabab wameendelea kutishia kumpindua rais Hassan Sheikh Mohamud, aliyeingia madarakani mwaka uliopita.

Al-Shabab kwa miezi kadhaa sasa wamepunguza makali yao ya mashambulizi mjini Mogadishu na miji mingine baada ya wanajeshi ya AMISOM kuchua miji yote waliyokuwa wanathibiti.

Hata hivyo, kundi hilo la Al-Shabab limefanikiwa kuchua tena uthibiti wa mji wa Hudur makao makuu ya eneo la Bakool mji waliouchukua siku ya Jumapili.

Kundi la Al-Shabab limeendelea kuwa tishio la usalama katika kanda ya Afrika Mashariki na kati hasa nchini Kenya na Uganda ambazo zimetuma wanajeshi wao chini ya mwavuli wa AMISOM kupamabana nao.