Wabunge wa Cyprus wakutana kwa dharura kujadili hali ya kudorora kwa uchumi
Wabunge nchini Cyprus wanakutana katika kikao cha dharura kujadili hali ya mtikisiko wa kiuchumi nchini humo na hatua ya serikali ya kutaka benki kuwazuia wateja wake kuchukua fedha zao.
Imechapishwa:
Serikali ya Cyprus imependekeza kuwa raia nchini humo walio na akaunti katika Benki mbalimbali wachangie kuimarisha hali ya kiuchumi nchini humo pendekezo ambalo limewakasirisha sana wananchi wa taifa hilo.
Ili kupitishwa kwa pendekezo hilo katika bunge hilo lenye wabunge 56 chama tawala cha rais Nicos Anastasiades kinahitaji uungwaji mkono kutoka kwa wabunge wengine ili kufanikiwa.
Cyrprus ipo katika mpango wa kubana matumizi ya fedha unaokadiriwa kuwa Euro Bilioni 10 kama ilivyokubaliwa na Umoja wa Ulaya na shirika la fedha duniani IMF.
Rais Anastasiades hata hivyo anasema kuwa, anafanya kila kilicho ndani ya uwezo wake kupunguza kiwango cha wateja wa Benki nchini humo kuchangia katika mpango huo ili kuzuia maandamnao nchini humo.
Serikali ya Urusi imesema pendekezo hilo la serikali ya Cyrprus kwa wananchi wake si kitu kizuri na pia ni hatari kwa uchumi wa taifa hilo.
Ikiwa pendekezo hilo litaungwa mkono na wabunge watakaopiga kura siku ya Jumanne Benki zote nchini humo zitafungwa ili kuwazuia raia nchini humo kutoa fedha kwenye akaunti zao.