VATICAN

Papa Francis aanza kazi rasmi atoa wito kwa watu na viongozi duniani kuwasaidia maskini

Kiongozi mpya wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis ameanza kazi ya kuwaongoza waumini Bilioni 1 nukta 2 wa Kanisa hilo kote duniani baada ya kuongoza misa maalum katika makao makuu ya Kanisa hilo mjini Rome  nchini Italia.

Matangazo ya kibiashara

Maelfu ya watu walikusanyika kumsikiliza Papa Francis ambaye alitoa wito kwa watu wote duniani pamoja na viongozi kuwajali watu maskini na wasiojiweza katika jamii.

Misa hiyo ilihudhuriwa pia na viongozi wa kisiasa pamoja na wale wa dini kutoka kote duniani  akiwemo Makamu wa rais wa Marekani Joe Biden, kiongozi wa Kanisa la Orthodox duniani Patriarch Bartholomew na rais wa Zimbabwe Robert Mugabe miongoni mwa wengine.

Bartholomew anakuwa kiongozi wa kwanza wa Kanisa la Orthodox  kuhudhuria uzinduzi wa Papa mpya wa Kanisa Katoliki ndani ya miaka 1,000 tangu kugawanyika kwa Kanisa hilo ambalo lilikuwa pamoja.

Papa Francis ni kiongozi wa kwanza wa Kanisa hilo kutoka kwa bara la Amerika na ameahidi mabadiliko makubwa katika Kanisa hilo kinyume na waliomtangulia katika wadhifa huo.

Kiongozi huyo alichaguliwa na Makadinali wa Kanisa hilo kutoka kote duniani wiki iliyopita na anachukua nafasi ya Benedicto wa kumi na sita aliyejiuzulu mwishoni mwa mwezi wa pili kwa sababu ya umri wake mkubwa pamoja na hali yake ya kiafya.

Papa Benedicto alikuwa kiongozi wa kwanza wa Kanisa hilo kujiuzulu wadhifa wake ndani ya miaka 600 baada ya kusema kuwa umri wake wa miaka 85 haungemruhusu kuendelea kuliongoza kanisa hilo.