Zimbabwe

Wananchi wa Zimbabwe waipitisha Katiba Mpya kwa asilimia 95

Asilimia 95 ya wananchi wa Zimbabwe waliipiga kura ya ndio kuunga mkono rasimu ya Katiba mpya nchini humo Jumamosi iliyopita.

Matangazo ya kibiashara

Matokeo ya mwisho ya kura hiyo ya maoni yalitangazwa siku ya Jumanne na tume ya Uchaguzi nchini humo na kuonesha kuwa watu 3,079,966 waliipitisha Katiba hiyo mpya huku watu 179,489 wakiipinga.

Mwenyekiti wa tume hiyo ya Uchaguzi Lovemore Sekeramayi ametangaza rasmi kuwa rasimu hiyo imepitishwa na wananchi wa Zimbabwe waliojitokeza kushiriki katika zoezi hilo.

Takriban watu Milioni sita walijisajili kupiga kura katika zoezi hilo la kihistoria nchini humo.

Viongozi wa serikali ya Muungano rais Robert Mugabe na Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai wote waliunga mkono Katiba hiyo mpya ambayo sasa itawezesha kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu mwezi Julai mwaka huu na kumalizika kwa serikali hiyo ya muungano .

Ikiwa Robert Mugabe mwenye umri wa miaka 89 atawania tena urais nchini humo ataweka historia kuwa kiongozi mkongwe zaidi barani Afrika kuwania urais.

Rais Mugabe ambaye amekuwa rais tangu mwaka 1980 pia ameunga mkono katiba hiyo mpya, na ikiwa atachaguliwa kwa mihula miwili ataongoza nchi hiyo kwa miaka kumi ijayo.

Katiba mpya inaruhusu rais kuongoza nchi hiyo kwa mihula miwili pekee na pia inalipa bunge nguvu ya kudhinisha uteuzi unaofanywa na rais.

Baada ya Katiba hiyo mpya kupitishwa itasainiwa na rais Robert Mugabe baada ya siku 30 ili kuanza kutumiwa rasmi .

Miongoni mwa vifungu muhimu vinavyopatikana ndani ya Katiba mpya nchini humo ni pamoja na wananchi wote wanalindwa dhidi ya mateso yeyote na kuwa na uhuru wa kujieleza .