SYRIA-UN-MAREKANI

UN na Marekani kuchunguza ikiwa silaha za kemikali zinatumiwa nchini Syria.

Marekani na Umoja wa Mataifa zinachunguza ikiwa kweli silaha za kemikali zinatumiwa nchini Syria wakati huu serikali na upinzani zikituhumiana kuhusu utumizi wa silaha hizo.

Matangazo ya kibiashara

Viongozi wa upinzani nchini Syria wameituhumu serikali  kwa kuamuru wanajeshi wake kutumia silaha hizo katika mji wa Allepo dhidi ya wapinzani na kusababisha mauaji ya watu 31 na zaidi ya 100 kujeruhiwa, madai yanayokanushwa vikali na serikali ya rais Bashar AL Assad.

Kamanda wa Majeshi ya Mataifa ya Magharibiu NATO James Stavridis, amesema kuwa ikiwa uchunguzi utabaini kuwa silaha za kemikali zinatumiwa huenda NATO ikaivamia Syria kijeshi.

Hata hivyo, Stavridis amesisitiza kuwa ni sharti Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lipitishe azimio la kutumwa kwa wanajeshi hao nchini humo kabla ya hatua kuchukuliwa .

Serikali ya Urusi inasema kuwa ina habari kutoka Damascus kuwa waasi walitumia silaha za kemikali  suala ambalo wanasema ikiwa ni kweli basi huenda machafuko nchini Syria yakawa mabaya zaidi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ameonya kuwa ikiwa kweli silaha hizo zinatumiwa huenda hali ikaendelea kudorora  lakini kwa sasa UN haiwezi kuthibitsiha  ikiwa kweli silaha hizo zitatumiwa.

Machafuko nchini Syria yameingia mwaka wa pili na kusabisha zaidi ya watu elfu 70 na maelfu ya watu kukimbia makwao.

Upinzani nchini Syria unataka rais Bashar AL Assad kuondoka madarakani, shinikizo ambazo zinaungwa mkono na mataifa ya Magharibi.